CAF yairahisishia kazi Yanga

Muktasari:
Hata hivyo ikiwa na bashasha za ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar juzi Jumamosi katika mechi ya kiporo, Yanga ni kama imerahisishiwa kazi ya kuiua Al Ahly kwa kupangiwa waamuzi kutoka nje ya Kanda ya Afrika Kaskazini.
YANGA ikiwa na mzuka wa ushindi wa mechi zake za viporo vya Ligi Kuu Bara, jana Jumapili imeifuata Al Ahly ya Misri kitemi, huku nyuma mabosi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wakiirahisishia kazi katika mechi yao ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa.
Mabingwa hao wa Tanzania, waliondoka jana kuwahi pambano lao la marudiano dhidi ya Waarabu hao litakalochezwa keshokutwa Jumatano ambapo Yanga inahitaji ushindi au sare ya kuanzia mabao mawili iweze kusonga mbele hatua ya makundi.
Hata hivyo ikiwa na bashasha za ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar juzi Jumamosi katika mechi ya kiporo, Yanga ni kama imerahisishiwa kazi ya kuiua Al Ahly kwa kupangiwa waamuzi kutoka nje ya Kanda ya Afrika Kaskazini.
Ipo hivi. CAF imewapangia Yanga waamuzi wa kuchezesha mechi na wenyeji wao kutoka nje ya Afrika Kaskazini, kitu ambacho kama itajituma uwanjani na kucheza kwa nidhamu ni lazima ivunje rekodi ambayo imekuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu.
Waamuzi watakaochezesha mchezo huo wanatokea Mali, kinyume na miaka ya nyuma ambapo mechi nyingi za timu za Kaskazini mwa Afrika za nyumbani zilichezeshwa na waamuzi kutoka ukanda huo ambao wanazungumza kiarabu na kufanana kitamaduni.
Suala hilo limekuwa likilalamikiwa mara nyingi kuwa limekuwa likichangia waamuzi hao kuzikandamiza timu pinzani katika matokeo ya mechi zao za nyumbani.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Caf, mwamuzi wa kati katika mechi hiyo itakayofanyikia Uwanja wa Borg El Arab jijini Alexandria ni Mahamadou Keita akisaidiwa na Balla Diarra na Drissa Kamory Niare wote kutoka Mali.
Hali iko tofauti kwa wawakilishi wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika, Azam ambao mechi yao ya marudiano dhidi ya Esperance nchini Tunisia, itachezeshwa na waamuzi kutoka nchini Morocco.
Waamuzi hao ni Rédouane Jiyed atakayesaidiwa na Mouhib Abdallah Filali na Essam Benbapa. Katika mechi ya kwanza Azam iliifunga Esperance mabao 2-1.
WANNE WATEMWA
Yanga iliondoka jana jioni kuelekea Misri ikiwa na msafara wa wachezaji 20, huku vifaa vyake vinne vikiachwa jijini Dar es Salaam kwa sababu mbalimbali.
Wachezaji walioachwa na Kocha Hans Pluijm jijini ni kipa Benedicto Tinocco, beki Haji Mwinyi aliye majeruhi, kiungo Geofrey Mwashiuya na mshambuliaji Matheo Antony.
“Wachezaji hao tumewaacha kwa sababu mbalimbali, lakini tuna imani ya kufanya vema ugenini,” alisema Kocha Msaidizi, Juma Mwambusi ambaye alifichua siri ya kwenda kuiua Al Ahly kwao.
MFUMO MPYA
Kama hukugundua ni kwamba katika mchezo wao na Mtibwa Sugar ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0, kikosi hicho kilitumia mfumo mmoja mgumu ambao uliwapa shida wapinzani wao.
Ukiondoa kipa Yanga ilianza nyuma na mabeki watatu Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani na Vicent Bossou, kati ikiwaweka kina Juma Abdul, Oscar Joshua, Thabani Kamusoko, Deus Kaseke na Haruna Niyonzima na mbele kulikuwa na Donald Ngoma na Simon Msuva.
Mwambusi alifichua kuwa Ngoma na Msuva walikuwa wakirudi chini na kufanya mfumo wao kusomeka 3-5-2 ambao ni maalum kwa kuzuia kwa nguvu na kushambulia kwa kushtukiza mfumo ambao mara ya mwisho Yanga iliutumia katika mchezo dhidi ya Simba na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Akielezea mfumo huo, Mwambusi amesema aina hiyo ya mfumo ulikuwa katika majaribio maalum katika kuelekea mchezo dhidi ya Al Ahly ambapo wanajua kwamba Waarabu hao watakuja kwa kasi katika dakika za mwanzo ambapo ukuta wao unatakiwa kuwa imara kuzuia kufungwa bao la mapema.
“Tulikuwa tunajaribu kuona kama mfumo huo utakuwa na faida kwetu lakini naona umetusaidia kwa kuwa hatukuruhusu bao unajua wale jamaa watakuja kwa kasi dakika za mwanzoni, tunatakiwa kuwa makini tusiruhusu bao, tumeona kilichofanyika na tutaenda kuweka mambo sawa kabla ya kuvaana na Al Ahly.”
PLUIJM HUYU HAPA
Bosi wa Mwambusi, Hans Pluijm akatamka kwamba mbali na mpango huo akili ya pili kwao ni kuhakikisha wanapata bao la mapema ambalo litawachanganya zaidi wapinzani wao lakini utamu zaidi mtaalamu huyo wa Kidachi akatamka kwamba tayari anao mkanda wa mchezo wa ligi dhidi ya ENPPI uliopigwa Ijumaa ya Aprili 15 na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
“Nimewaangalia wanavyocheza nyumbani katika ligi, kuna kitu kimenipa faraja ambacho nitawaelekeza vijana, muhimu ni kuhakikisha kama tutafanikiwa kupata bao la mapema na hilo linawezekana kama tukitanguliza akili kwa kutulia katika mashambulizi yetu,” alisema Pluijm.
REKODI TATA
Yanga inaenda kuvaana na Al Ahly ikiwa ina rekodi mbaya ugenini dhidi ya Waarabu, tangu mwaka 1982 ilipokutana na Al Ahly, Yanga haijawahi kushinda ugenini zaidi ya sare ya 1-1 dhidi ya Ismailia pia ya Misri mwaka 1992.
Katika safari zake 10 nyingine kwa timu za Afrika Kaskazini, Yanga imekuwa ikichezea nyingi, jambo ambalo wanayanga wanaamini mwaka huu inatosha, lifikie tamati.