Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Buriani Epaphra Amana Swai

Muktasari:

Taarifa za kifo cha Swai aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hadi anafikwa na mauti nilizipata Alhamisi, Januari 28 mwaka huu saa 4 asubuhi.

NI majonzi. Si kwa wale tu waliowahi kufanya kazi na Epaphra Amana Swai (57), bali kwa familia na wadau wa soka nchini.

Taarifa za kifo cha Swai aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hadi anafikwa na mauti nilizipata Alhamisi, Januari 28 mwaka huu saa 4 asubuhi.

Alifikwa na mauti kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na alikuwa amehamishiwa kutoka Hospitali ya Kairuki iliyopo Mikocheni kwa ajili ya kupata matibabu zaidi.

Mara ya mwisho kuzungumza na Swai ilikuwa saa 8 mchana ya Alhamisi ya Januari 19 mwaka huu, baada ya kupewa taarifa na Katibu wa Chama cha Soka wa Shinyanga (SHIREFA), Mwalimu Nassoro kuwa alikuwa mgonjwa.

Nilizungumza naye kwa simu kwa sekunde 25 tu, akiwa Uwanja wa Ndege jijini Mwanza kuja Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu na aliniambia alikuwa anaumwa sana. Kumbe ndiyo nilikuwa naisikia kwa mara ya mwisho sauti ya Swai niliyefahamiana naye miaka 18 iliyopita kupitia soka.

Wakati huo, Swai alikuwa Katibu Mkuu wa timu ya Pamba-Mwanza maarufu kama TP Lindanda, nami nikiwa Mwandishi wa Michezo wa gazeti la kila siku la Majira. Ukaribu naye ulitokana na ushirikiano aliokuwa akinipa kila nilipowasiliana naye kutaka kujua mambo ya utawala yanayoendelea katika timu ya Pamba.

Swai ambaye alizikwa Jumamosi, Januari 30 mwaka huu nyumbani kwao Machame mkoani Kilimanjaro, hakuwa mjivuni kwa masuala ya soka, licha ya kuutumikia mchezo huo katika ngazi mbalimbali za uongozi kwa zaidi ya miaka 20.

Alipata Elimu ya Sekondari katika Shule ya Moshi Technical mkoani Kilimanjaro kuanzia mwaka 1977 hadi 1980. Pia alikuwa mtaalamu wa masuala ya ukaguzi (Auditing), sifa ambayo bila shaka ilimfanya mwaka 2008 ateuliwe kuwa Mjumbe wa Kamati ya Ukaguzi ya Hesabu za Ndani ya TFF.

Mbali ya Pamba, Swai aliyekuwa mwajiriwa wa Bodi ya Pamba akiwa Mkaguzi wa viwanda vya pamba kwa Kanda ya Magharibi, alipata pia fursa ya kuongoza akiwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Wilaya ya Nyamagana (NDFA) na Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA).

Pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Toto Africans na Mwenyekiti wa Chama cha Soka Wilaya ya Bariadi (BFA). Mbali ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, wadhifa mwingine aliokuwa nao hadi anafikwa na mauti ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Simiyu (SIFA).

Aliiongoza SIFA ikiwa na changamoto nyingi, kwani alikuwa ndiye Mwenyekiti wa kwanza cha chama hicho katika mkoa huo mpya wa Simiyu. Uzoefu wake pamoja na ushauri kwa viongozi wa wilaya, klabu na mdau mmoja mmoja ulisaidia kuisimamisha SIFA.

Ilikuwa ni kawaida ya Swai kila uliposalimia naye, jambo la kwanza ni kukupa pole ya kazi. Salamu ya pole kwa kazi kutoka kwa Swai kwenda kwa wenzake katika soka haikuwa na jambo lingine zaidi ya kutambua mchango wao katika maendeleo ya mchezo huo.

Ushirikiano na ukaribu zaidi kwangu uliongezeka baada ya Swai kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27 mwaka 2013 jijini Dar es Salaam, hivyo kuwa bosi wangu wakati huo nikiwa Ofisa Habari ndani ya Shirikisho.

Swai aliibuka mshindi katika nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji akiwakilisha Kanda namba tatu ambayo ni mikoa ya Shinyanga na Simiyu. Nafasi hiyo ni moja kati ya zile zilizokuwa na mchuano mkali kwani alitenganishwa kwa kura mbili tu na mpinzani wake. Alipata kura 63 dhidi ya 61 za mpinzani wake Mbasha Matutu Mong’ateko.

Licha ya ushirikiano na kutoa ushauri, Swai alikuwa na hulka moja kubwa. Asipokubaliana na utaratibu wa uongozi katika soka, hatua inayofuata ilikuwa ni kujiuzulu. Alifanya hivyo katika klabu ya Pamba na hata MZFA.

Haikuwa rahisi kubaini utendaji na umahiri wake katika uongozi kama hukuwa karibu naye au kufanya naye kazi mara kwa mara, kwani hakuwa kiongozi mwenye kutanguliza mbele sifa na majivuno.

Nilipoteuliwa na Kamati ya Utendaji kuwa Mkurugenzi wa Mashindano TFF, aliniambia ana matumaini makubwa nami. Lakini kubwa ninalokumbuka ni jinsi alivyonipa moyo na kunieleza kuwa kwa anavyonifahamu nitaweza kuifanya kazi hiyo bila matatizo.

Swai alikuwa zaidi ya mtu wa kutafuta ufumbuzi, lakini zaidi kutengeneza suluhu ili kujenga mazingira ya ustawi wa soka. Si tu ametangulia, lakini tayari ameshafanya yake hapa duniani, hasa kwa soka la Tanzania. Sisi sote ni waja wake Mola. Hakika kwake tutarejea. Tangulia Swai tutakukumbuka daima kwa mchango wako, nasi tu nyuma yako.

Mwandishi ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)