Bondia Mtanzania adundwa TKO Ulaya

Muktasari:

  • Nasibu alikumbana na kipigo hicho katika sekunde ya 28 ya raundi ya tano katika pambano la raundi 10 la uzani wa feather dhidi ya James Dickens.

Dar es Salaam. Bondia Nasibu Ramadhan ameshindwa kutwaa ubingwa wa Jumuiya ya Madola baada ya kukubali kipigo cha Technical Knock Out (TKO).

Nasibu alikumbana na kipigo hicho katika sekunde ya 28 ya raundi ya tano katika pambano la raundi 10 la uzani wa feather dhidi ya James Dickens.

Katika pambano hilo lililopigwa usiku wa kuamkia jana kwenye Ukumbi wa Olympia, Liverpool, England, refarii Mark Lyson alilazimika kusimamisha pambano hilo.

“Niliumia hivyo sikuweza kuendelea na pambano,” alisema Nasibu muda mfupi baada ya pambano hilo lililosimamiwa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Uingereza (CBBC).

Promota wa ngumi nchini, Shomari Kimbau alisema Nasibu alielemewa na konde la mpinzani wake.

“Alipigwa punch ya kushoto ambayo ilimkuta juu ya sikio ikamlevya, lakini ukiangalia hilo pambano ni kama Nasibu alichoka mapema, hakuwa na spidi ile iliyozoeleka,” alisema.

Alisema Nasibu alitoka kucheza wiki mbili zilizopita nchini Namibia.