Bomu la Atomic laua Wazee wa Kazi

OSCAR KAKAI, BUNGOMA KIKOSI cha Atomic FC kimeirarura Wazee Wa Kazi FC kwa kuifunga mabao 2-1 katika mechi ya kupimana nguvu ambayo ilichezwa katika Uwanja wa Shule ya Msingi Khayo MMK. Mechi hiyo ilianza kwa kasi huku bao la kwanza likipachikwa wavuni dakika ya 8 kupitia mshambuliaji Geofrey Oniango. Bao la pili lilisukumwa kimiani dakika ya 69 kupitia kwa Francis Opili. Bao la Wazee Wa Kazi lilifungwa na John Alwaka katika dakika ya 76. Mechi hii ilileta mashabiki wengi uwanjani humo. Kocha wa Atomic, Sabastiana Otsula, alisema kuwa timu hiyo inajipanga kwenda kumenyana na The Stars ya nchini Uganda wiki ijayo. Otsula alisema kuwa timu hiyo iko ngangari na imefanya mazoezi ya kutosha ili iweze kutoana jasho na wenyeji wao hao wa Uganda.