Bocco: Tulieni, Tunamaliza

Muktasari:

MASTAA wa Simba jana usiku walitua salama kwenye ardhi ya Botswana huku nahodha John Bocco akisisitiza kwamba; “Tumejipanga na tunataka kumaliza kazi.”

MASTAA wa Simba jana usiku walitua salama kwenye ardhi ya Botswana huku nahodha John Bocco akisisitiza kwamba; “Tumejipanga na tunataka kumaliza kazi.”

Bocco aliweka wazi wao kama wachezaji wanatambua ugumu wa mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy itakayochezwa saa 9 za Botswana sawa na saa 10 kwa Tanzania.

“Msimu huu tumejipanga zaidi kuliko msimu uliopita, tunajua tunaenda kucheza na timu nzuri lakini tunaamini tutafanya vizuri na kushinda mechi,” alisema Bocco atakayeanza kikosi cha kwanza kesho kwa mujibu wa mazoezi ya Kocha Didier Gomes.

“Tumejifunza kutokana na michezo ya nyuma ya mashindano haya na sasa tumejipanga kuendeleza tulipoishia msimu uliopita,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Azam.

Mwanaspoti linajua kuwa hata kabla ya kuwasili kwa kikosi kizima Botswana, Simba tayari ilikuwa imetuma Jeshi la watu kadhaa akiwemo mratibu wa chama hilo, Abas Ally kuandaa mazingira ambaye aliambatana na mpishi.

Ili kuhakikisha wanaruka vihunzi vya fitina za ugenini, moja ya vigogo wa Simba alilipenyezea Mwanaspoti kuwa wamechukua Hoteli yenye ulinzi mkali na kila kitu watafanya wao Simba ikiwemo misosi, usafiri na hata maji ya kunywa watatumia ya kwao.

“Nimeiona Galaxy ni timu nzuri yenye wachezaji bora kila idara, nimeusoma mchezo wao na kuufanyia kazi mazoezini na nadhani itakuwa ni mechi ngumu lakini tumejipanga kushinda ugenini na kumaliza kazi kule kwani uwezo huo tunao,” alisema Gomes ambaye ni raia wa Ufaransa mwenye wasaidizi wawili kwenye benchi lake.

Wachezaji waliokuwepo mazoezi ya mwisho ni
AbdulSamad Kassim, Meddie Kagere, Erasto Nyoni, Sadio Kanoute, Mohamed Hussein, Shomary Kapombe, Rally Bwalya, Thadeo Lwanga, Hennoc Inonga, Pascal Wawa, Muzamiru Yassin, Jonas Mkude na Benard Morrison. Wengine ni Joash Onyango, John Bocco, Kibu Denis, Yusuph Mhilu, Israel Mwenda, Kennedy Juma, Ahmed Feruz, Aishi Manula, Jeremiah Kisubi na Beno Kakolanya.

Kama kawaida walianza kwa kupasha misuli kwa dakika kama 10 hivi baada ya hapo kila mtu alipewa mpira wake na kuanza kupiga danadana na kontro kadhaa.
Kilichofuata Gomes alipanga mabeki viungo, mawinga na washambuliaji katika nusu ya Uwanja na kuanza kuelekeza namna ya kupiga pasi katika maeneo na kutafuta nafasi. Muda huo mabeki wote wakiongoza na Wawa walikuwa na program yao maalumu ya kuanzisha mipira na mazoezi hayo yalidumu kwa dakika 20.

Baada ya hapo walibadili uchezaji na kupanga koni zilizotengeneza kama msitatiri katikati ya uwanja na kuunda timu mbili zilizokuwa zinacheza kwa kukabana maarufu zubaisha bwege zoezi lililodumu kwa dakika zisizopongua 10. Baada ya hapo waliweka magoli katikati ya uwanja na kuanza kucheza kama mechi zoezi lililodumu kwa dakika 25 na kuzalisha bao moja pekee lililofungwa na Kibu Denis.

Timu ya kwanza ilikuwa na Manula, Kapombe, Tshabalala, Wawa, Kennedy, Kanoute, Lwanga, Morrison, Bwalya, Dilunga na Bocco huku timu ya pili ilikuwa na Kakolanya, Mwenda, Mkude, Varane, Onyango, AbdulSamad, Mhilu, Muzamiru, Kagere, Kibu na Nyoni.

Kwa namna mazoezi yalivyokuwa, Simba ilionekana kukomaa na mbinu za kucheza kwa kujilinda na kushambulia kwa kushitukiza huku ikitumia mawinga wenye mbio, Morrison, na Dilunga.