Bocco kama Mziba tu

MWENDELEZO wa kiwango bora cha nahodha wa Simba na Taifa Stars, John Bocco umetazamwa kwa jicho la kiufundi, kimbinu na staa wa zamani wa Yanga, Abeid Mziba.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mziba alisema kuwa Bocco ni mchezaji mwenye mtazamo komavu na kazi yake, anayetambua majukumu na kujijengea heshima kubwa kwenye soka nchini.

“Mastraika wengi wazawa wamefunikwa na wageni, ila ni tofauti na Bocco ambaye heshima yake ipo ndani ya kikosi cha kwanza tofauti na wachezaji wengine wanaoibuka na kupotea,” alisema.

Alisema laiti kama wachezaji wengine wangekuwa wanatunza viwango vyao kama Bocco, Taifa Stars isingekuwa na uhaba wa washambuliaji wa kupata matokeo mazuri kwenye mechi ngumu na nyepesi zinazoikabili timu hiyo.

“Kuna washambuliaji wengi ila wanafunikwa na wachezaji wa kigeni. Hata ukiangalia kwenye msimamo wa wafungaji anayeongoza ni Prince Dube wa Azam mabao 12, Meddie Kagere mabao 11 wa Simba na Bocco 10.”

Mbali na Bocco, pia Mziba alimtaja Ditram Nchimbi wa Yanga kwamba licha ya kutokuwa kwenye wakati mzuri wa kufunga kama ilivyo hamu ya mashabiki wake anamuona ni straika mzuri kama atapata utulivu wa kujua nini anatakiwa kufanya uwanjani.

“Nchimbi ni straika mzuri, akituliza akili yake atafanya makubwa, ndiye aliipa ushindi Stars kwenda Afcon, kwangu namwamini, ushauri ni kutuliza akili yake tu.” Kwa wachezaji wa kigeni alimkingia kifua Michael Sarpong kwamba wampe msimu mwingine atakuwa amezowea ligi na kinachomfurahisha kwa staa huyo ni umiliki wa mpira.

“Ukiniambia nitaje washambuliaji wa kigeni ni Sarpong, Chriss Mugalu, Kagere tayari uwezo wake unajulikana huko kukaa benchi ni vitu vinavyoweza kumtokea mchezaji yoyote,” alisema.