Big six yashikwa koo

Muktasari:

Man United ilivuna Pauni 275 milioni mwaka 2019 kutoka kwenye dili za kibiashara, ikiwamo Pauni 173 milioni kutoka kwa wadhamini. Man City, Liverpool na Chelsea zote zilivuna zaidi y Pauni 180 milioni kupitia dili za kibiashara, huku Spurs ikivuna Pauni 135 milioni na Arsenal Pauni 111 milioni.

LONDON, ENGLAND . KINACHOELEZWA ni kwamba Juventus wanapasua kichwa juu ya supastaa wao, Cristiano Ronaldo wambakize au wamuuze tu msimu utapokwisha ili kupunguza bili ya mishahara wanayopaswa kumlipa. Ronaldo analipwa zaidi ya Pauni 500,000 kwa wiki na janga la virusi vya corona limeleta mtikisiko mkubwa kwenye uchumi wa klabu za Ulaya.

Kitu kama hicho kinaweza kuzikumba klabu za Big Six kwenye Ligi Kuu England, baada ya kudaiwa kwamba huenda zikaingia kwenye mgogoro mkubwa wa kiuchumi kutokana na kukosa pesa za wadhamini baada ya janga hilo la corona. Liverpool, Manchester United, Manchester City, Arsenal, Chelsea na Tottenham wapo kwenye hatari ya kupoteza mkwanja wa Pauni 3 bilioni ikiwa ni mapato ya kutoka kwenye dili za televisheni. Kuna mamilioni mengine mengi tu yatapotea kutoka kwenye mapato yao ya dili za kibiashara, hasa udhamini. Bosi mmoja wa kutoka timu hizo, amesema jambo hilo punde litakuwa tatizo kubwa kwenye timu.

Man United ilivuna Pauni 275 milioni mwaka 2019 kutoka kwenye dili za kibiashara, ikiwamo Pauni 173 milioni kutoka kwa wadhamini. Man City, Liverpool na Chelsea zote zilivuna zaidi y Pauni 180 milioni kupitia dili za kibiashara, huku Spurs ikivuna Pauni 135 milioni na Arsenal Pauni 111 milioni.

Sasa janga la corona linaweza kupeperusha pesa zote hizo na kuziacha klabu kwenye hali mbaya ya kumudu gharama kulipa mishahara ya wachezaji wao inaowalipa mkwanja mrefu na huenda wakaangukia kwenye sakata la Juventus na Ronaldo. Kama ikitokea ishu ya kupunguza wachezaji wanaolipwa mishahara mikubwa kwenye klabu za Big Six Ligi Kuu England, basi kuna masta hao itakula kwao.

Kwenye kikosi cha Chelsea kuna mastaa kama Jorginho, anayelipwa Pauni 102,000 kwa wiki na Kepa Arrizabalaga, Pauni 192,000 kwa wiki. Kwa muda sasa, Kepa anatajwa kuwa na kiwango kibovu golini na kuhusishwa na mpango wa kuuzwa, huku Jorginho akidaiwa kuwa ni mchezaji wa Maurizio Sarri na anaweza kurudi kumsajili.

Man City ina mastaa kama Kevin De Bruyne, anayelipwa Pauni 350,000 kwa wiki na Raheem Sterling, Pauni 300,000 kwa wiki. Man City yenyewe ipo kwenye hatari ya kukosa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu miwili, ukichanganya hasara itakayopatikana kwenye corona, inaweza kufungulia milango mastaa wake kibao ikionekana kuna shida kwenye kumudu mishahara yao.

Liverpool inaweza kufungulia milango ya kutokea mastaa wake, Mohamed Salah, anayelipwa Pauni 200,000 kwa wiki na Roberto Firmino, Pauni 180,000 kwa wiki, huku Spurs ikiwa na wakali kama Harry Kane, anayelipwa Pauni 200,000 kwa wiki na Tanguy Ndombele, Pauni 200,000 kwa wiki, huku kwenye kikosi cha Arsenal, wachezaji ambao wanaweza kufunguliwa milango ya kutokea ni Mesut Ozil, anayelipwa Pauni 350,000 kwa wiki na Pierre-Emerick Aubameyang, Pauni 200,000 kwa wiki, wakati Man United mastaa wake wanaolipwa pesa nyingi ni kipa David de Gea, Pauni 375,000 kwa wiki, Alexis Sanchez, Pauni 505,000 kwa wiki na Paul Pogba, Pauni 290,000 kwa wiki.

Mastaa wote hao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakihusishwa na mpango wa kuzihama timu zao na huenda jambo hilo litatimia wakati huu kutokana na timu kujaribu kupunguza gharama, huku timu kama Man United ikifikiria kumrudiha kipa wao aliye kwa mkopo Sheffield United, Dean Henderson.