Biashara United yalamba udhamini mnono

Muktasari:
Taarifa iliyowekwa kwenye ukurasa rasmi wa mtandao wa Instagram ya timu hiyo inaitangaza kampuni ya Barrick North Mara Gold Mine kuwa ndiye mdhamini mkuu wa klabu hiyo.
Mwanza. Umasikini ndani ya klabu ya Biashara United utakuwa historia baada ya Kampuni ya Barrick North Mara Gold Mine kuamua kuidhamini timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima aliyefanikisha kupatikana kwa udhamini huo alisema taarifa zaidi juu ya makubaliano watafutwe viongozi wa klabu hiyo kwa ufafanuzi zaidi.
“Mimi ni mdau mkubwa wa michezo na timu ya Biashara United ambayo iko mkoani kwangu, napenda maendeleo ya mpira kwahiyo kupatikanaji kwa mdhamini kuitasaidia siyo tu timu yetu, bali pia kutainua kiwango cha soka,”alisema Malima.
Walipotafutwa viongozi wa klabu hiyo, Mwenyekiti Seleman Mataso na Katibu wake Mkuu, Hajji Mtete hawakupatikana kulizungumzia suala hilo.
Hata hivyo, mmoja wa viongozi ndani ya Klabu hiyo ambaye hakutaka kuandikwa jina lake, aliithibitisha kampuni hiyo imeweka mezani kitita cha zaidi ya Sh200 milioni kwa ajili ya kulipa mishahara ya wachezaji na benchi la ufundi.
“Fedha hizo zitatumika kulipa mishahara kwa wachezaji na benchi la ufundi. Habari kamili zitatolewa kesho Ijumaa, lakini kila kitu kimekamilika,” alisema kiongozi huyo
Hata hivyo, taarifa iliyowekwa kwenye ukurasa rasmi wa mtandao wa Instagram ya timu hiyo inaitangaza kampuni ya Barrick North Mara Gold Mine kuwa ndiye mdhamini mkuu wa klabu hiyo.
Pia kama haitoshi, katika mchezo uliopita kati ya Biashara United na Simba wachezaji wa timu hiyo walikuwa wamevalia jezi zenye nembo ya kampuni hiyo kifuani licha ya kulala mabao 2-0.