Beno atoweka kambini muda mchache kabla ya Singida kuivaa Yanga

Muktasari:

  • Beno ametoweka kambini ikiwa ni muda mchache uliobaki kwa kikosi hicho cha Singida kinachokabiliwa na mchezo wake wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga unaopigwa leo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni.

KLABU ya Singida Fountain Gate imetoa taarifa ya kusikitishwa kwa kitendo kilichoonyesha na kipa wa timu hiyo, Beno Kakolanya cha kutoweka kambini.

Beno ametoweka kambini ikiwa ni muda mchache uliobaki kwa kikosi hicho cha Singida kinachokabiliwa na mchezo wake wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga unaopigwa leo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni.

Taarifa iliyotolewa na Singida kwa vyombo vya habari ilieleza; "Klabu ya Singida Fountain Gate FC inasikitishwa na kitendo cha mchezaji wetu, Beno Kakolanya kutoroka kambini tukiwa tunakabiliwa na mchezo muhimu kabisa dhidi ya Yanga leo,"

"Kitendo hiki kinaleta maswali mengi hasa ukizingatia kuwa Beno ni mchezaji mzoefu na mmoja wa wachezaji wa kutumainiwa wa timu ya Taifa. Tunaendelea kufuatilia taarifa zake na wachezaji wengine wowote watakaoonekana kuihujumu timu yetu kwenye mechi ya leo na nyingine zinazofuata."

Kipa huyo alijiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Simba huku akiwahi pia kuichezea Yanga inayocheza na Singida jioni ya leo.