Benchikha atambulishwa rasmi, aomba sapoti ya mashabiki

Muktasari:

  • Kocha huyo aliyeachana na USM Alger ya kwao Algeria baada ya kuipa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika na Super Cup alitua Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo Novemba 28

KLABU ya Simba imemtambulisha rasmi kocha mkuu wa kikosi hicho, Abdelhak Benchikha kwa ajili ya kuiongoza timu hiyo katika michuano mbalimbali msimu huu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Imani Kajula amesema wameingika mkataba wa miaka miwili na kocha huyo huku wakiwa na imani kubwa juu yake.

"Tulipokea CV za makocha wengi lakini tulikaa sisi kama viongozi tukajiridhisha anatufaa kwa ajili ya timu yetu hivyo niwaombe mashabiki zetu waendelee kumuunga mkono katika majukumu yake," amesema.

Aidha Kajula aliongeza, hawatomuingilia kocha huyo katika majukumu yake hivyo yeye ndiye atakayeamua mchezaji wa kucheza kwenye mchezo wowote  na sio vinginevyo.

Kwa upande wa Benchikha amesema amefurahi kupata nafasi ya kuiongoza timu hiyo huku akiomba ushirikiano kutoka kwa mashabiki.

"Kuanzia awali nilipoingia majadiliano na Simba nilifurahi sana na nashukuru kufanya kazi hapa Tanzania kwani ni nchi yenye amani na utulivu," amesema.

Kuhusu malengo ya timu, Benchikha amesema ni mapema sana kuzungumzia hayo ingawa anaamini kuna mambo mazuri yatakuja ndani ya kikosi hicho anayoenda kuyafanyia kazi kwa haraka.

"Nimekubali kuchukua timu katikati ya msimu lakini siwezi kuweka wazi ni mchezaji gani kwa sasa hafai au anafaa kikosini hadi pale nitakapoanza kufanya kazi rasmi," amesema.

Benchikha alitangazwa kujiunga na kikosi hicho Novemba 24 mwaka huu baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Roberto Oliveira 'Robertinho' kutimuliwa Novemba 7, mwaka huu ikiwa ni siku chache tu tangu Simba ikumbane na kichapo cha mabao 5-1, dhidi ya Yanga.

Kocha huyo aliyeachana na USM Alger ya kwao Algeria baada ya kuipa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika na Super Cup alitua Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo Novemba 28 akiwa na wasaidizi wake, Kocha msaidizi, Farid Zemiti na kocha wa viungo Kamal Boudjenane.