Benchikha anyoosha mkono bandarini, aibua maneno

Muktasari:

  • Mara ya mwisho Simba kuweka kambi Zanzibar ilikuwa siku chache zilizopita ikijiandaa na mchezo wa robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ambao ilipoteza kwa bao 1-0 kwa Mkapa.

KOCHA wa Simba, Abdelhak Benchikha ameonyesha mkono 'vidole vitano' wakati akiondoka na kikosi chake jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kwenda Zanzibar ambako wataweka kambi ya kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao utachezwa  Jumamosi ijayo dhidi ya Yanga.

Benchikha ndiye aliyekuwa wa kwanza kushuka katika gari dogo binafsi akiwa na wasaidizi wake wa benchi la ufundi saa 5:11 asubuhi kabla ya dakika chache baadaye basi la timu kuwasili feri mjini Dar es Salaam. Timu hiyo imesafiri kwenda Zanzibar kwa meli

Wakati Benchikha na wachezaji wake wakiingia kwenye geti kwa ajili ya safari ya kwenda Zanzibar, kulikuwa na baadhi ya mashabiki wa Simba na Yanga katika eneo hilo.

Wapo ambao walikuwa wakishangilia, wakizomea na wengine walikuwa wakitazama tu kinachoendelea.

Ndipo Benchikha alipoonyesha mkono wapo ambao waliona kocha huyo amelenga kuwasalimia tu na wengine waliona amedhamiria kurudisha mabao matano ambayo waliruhusu katika mchezo ambao walikutana na watani zao hao katika mzunguko wa kwanza.

Tukio hilo liliwafanya mashabiki wa Yanga kuzomea msafara wa Simba huku wengine wakidai wanachofuata Zanzibar, sio utulivu kama ambavyo ilielezwa bali ni masuala mengine ili kuhakikisha wanapata ushindi Jumamosi.

Simba imeondoka na wachezaji wake muhimu wa kikosi cha kwanza, akiwemo kipa chaguo la kwanza kwa sasa, Ayoub Lakred ambaye alikosekana katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu dhidi ya Ihefu uliopigwa Singida.

Watani hao wa jadi watakutana Jumamosi ikiwa ni mechi muhimu ambayo ina nafasi kubwa kwa timu hizo katika vita ya kuwania ubingwa wa ligi. Yanga inaongoza msimamo ikiwa na pointi 55 huku Simba ikiwa nafasi ya tatu na pointi 46.