Benchikha afumua kikosi, Kibu apewa msala

SIMBA chini ya kocha mkuu, Abdelhack Benchikha tayari imeweka wazi kikosi kitakachoikabili Al Ahly kwenye mechi ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika itakayopigwa kuanzia saa 3:00 usiku, Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Katika kikosi hicho, kuna mabadiliko kadhaa lakini kubwa zaidi ni eneo la ushambuliaji na Benchikha ameanza bila mchezaji asilia wa eneo hilo.

Eneo hilo la mbele, wameanzishwa viungo wawili washambuliaji, Saidi Ntibazonkiza na Clatous Chama pamoja na Kibu Denis ambaye kiasili ni winga.

Mastraika wa Simba ambao asili yao ni eneo la mbele kati (Namba Tisa), Pa Omary Jobe na Freddy Michael wote wameanzia benchi kwenye mechi hiyo.

Hivyo huenda mmoja kati ya Kibu na Saido akacheza kama namba tisa kwenye mechi hiyo ambayo Simba imedhamiria kushinda.

Wachezaji wengine watakaoanza ni kipa Ayoub Lakred, mabeki Mohamed Hussein, Shomary Kapombe, Che Malone Fondoh na Henock Inonga sambamba na viungo Babacar Sarr, Fabrice Ngoma na Sadio Kanoute.

Katika benchi wapo, Ally Salim, David Kameta, Israel Mwenda, Kennedy Juma, Willy Onana, Luis Miquissone, Mzamiru Yassin, Freddy na Jobe.

Simba inahitaji ushindi kwenye mechi hiyo ili kutanguliza mguu mmoja nusu fainali kabla ya mechi ya marudiano itakayopigwa Aprili 6, mwaka huu Misri.

Rekodi zinaibeba Simba kwenye mchezo huo kwani katika mechi tatu zilizopita ilipocheza na Al Ahly katika Uwanja wa Mkapa, Wekundu wa Msimbazi walishinda mbili na kutoa sare moja.