Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Beki Azam aandika rekodi mbili Bara

Muktasari:

  • Lusajo alifunga bao katika dk6, akiunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Abdul Suleiman ‘Sopu’ aliyetupia la pili dk16, huku Gibril Sillah akitupia jingine katika dk19, Nassor Saadun dk26 na Franck Tiesse dakika ya 53.

BAO moja lililofungwa na beki wa Azam FC, Lusajo Mwaikenda katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 5-0, dhidi ya Dodoma Jiji, Mei 13, 2025, limemfanya nyota huyo kuandika rekodi mbili muhimu, huku akiwa na msimu bora na timu hiyo hadi sasa.

Lusajo alifunga bao katika dk6, akiunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Abdul Suleiman ‘Sopu’ aliyetupia la pili dk16, huku Gibril Sillah akitupia jingine katika dk19, Nassor Saadun dk26 na Franck Tiesse dakika ya 53.

Sasa rekodi mbili alizoweka nyota huyo, mojawapo ni ya beki wa Ligi Kuu mwenye mabao mengi zaidi baada ya kutupia sita, huku nyingine ni ya kuivuka ya msimu wa 2020-2021, alipokuwa akikichezea kikosi cha KMC FC, alichokifungia mabao matano.

Lusajo ameivunja rekodi ya msimu uliopita, ambapo beki aliyekuwa na mabao mengi zaidi alikuwa ni Mrundi Derrick Mukombozi wa Namungo FC aliyefunga manne.

Mbali na Mukombozi, mwingine aliyefunga mabao mengi zaidi msimu uliopita ni Nicholas Gyan anayemudu kucheza namba mbili na wakati mwingine akicheza kama winga wa kulia akiichezea Singida Fountain Gate aliyemaliza msimu pia na mabao manne.

Msimu huu wanaomfuatia Lusajo ni Ibrahim Hamad ‘Bacca’ wa Yanga mwenye manne, sawa na Erasto Nyoni (Namungo), huku Shomari Kapombe (Simba), Pascal Msindo (Azam) na Hernest Malonga Singida Black Stars wakifunga matatu kila mmoja.

Wengine ni wenye mabao mawili ambao ni Wilson Nangu wa JKT Tanzania, Che Malone Fondoh (Simba), Yoro Diaby (Azam FC), Israel Mwenda (Yanga), Heritier Lulihoshi (Dodoma Jiji) na Mkongomani Andy Bikoko wa Tabora United.

Kwa sasa Lusajo anadaiwa mabao mawili ili kuifikia rekodi iliyowekwa na beki Shomari Kapombe msimu wa 2015-2026 alipoifunga mabao manane, ambayo haijawahi kufikiwa hadi sasa licha ya kasi ya mabeki wengine kufunga mabao.

Lusajo ana nafasi ya kuifika na kuivunja rekodi hiyo ya Kapombe, kama atafanya kweli katika mechi mbili zilizosalia kwa kikosi cha Azam dhidi ya Fountain Gate na Tabora United zitakazopigwa Juni 18 na 22.

Akizungumzia kiwango hicho, Lusajo alisema hakutegemea kama angefunga idadi kubwa ya mabao kama hayo msimu huu, ingawa jambo analozingatia ni kuisaidia timu.

“Kiukweli huwa nacheza na akili za wapinzani wetu kwa sababu napenda kuona timu yetu inapata matokeo mazuri, nikiona tu fursa ya kushambulia huwa nafanya hivyo, nashukuru benchi la ufundi linanisapoti na ninafanya kwa vitendo kama nahodha.”