BAZENGA GOR AWATAKA MAFANS KU-RELAX

BAZENGA wa Gor Mahia, Ambrose Rachier kawaomba mashabiki wa klabu hiyo kuwa watulivu huku akiahidi kubadilisha matokeo ya timu.
Msimu huu, Gor wameonekana kutotabirika. Leo wanashinda kesho wanapigwa keshokutwa wanatoka sare na mambo yamekuwa kama hivyo. Wamekosa konsistensi kama ilivyo Manchester United.
Kichapo cha juzi Jumapili mikononi mwao Wazambia Napsa Stars katika uwanja wa Kasarani ndio umewachefua zaidi mashabiki ambao wameelezea hasira yao kuhusu matokeo yanayozalishwa na Gor toka msimu huu ulipoanza.
Kwenye ligi kuu wanakamata nafasi ya  sita huku kwenye dimba la CAF Conferedation Cup waliyojikutamo baada ya kuchemsha kwenye Champions League, nayo wanaonekana ni kana kwamba huenda wakachujwa.
Hasira za mashabiki wa Gor sasa wamemwelekezea mwenyekiti Rachier wanayemkashifu kwa maandalizi mabaya ya timu pamoja na kile wanachodai kuwa alisaini wachezaji hafifu kabla ya kuanza kwa msimu huu.
Lakini Rachier anawataka mashabiki watulie, akisisitiza kwamba ni mapema mno kwa mashabiki kuanza kukosa imani na kikosi walichonacho.
“Kwa kweli hatukutegemea kupoteza ile mechi ya wikendi ila ndio hali ya mchezo na mashabiki wanalielewa hili. Hata kule majuu tumeziona timu kubwa zikichapwa na timu ndogo. Mbona wakati tunaposhinda huwa hatukemewi. Ni vyema kusapoti kikosi chetu katika hali zote.” Rachier kajikingia.
Na je kuhusu madai ya kuwa alisaini wachezaji wanyonge?
“Nimewasikia baadhi ya watu wakidai tulitumia fedha vibaya kwenye usajili tuliofanya. Nawahakikishieni kwamba sio kweli. Wachezaji tulioleta wana ubora na viwango na wanahitaji muda na watawashangaza, Hata  naye kocha wetu ni mzoefu ila anahitaji muda na kikosi na mambo yatakuwa sawa hivyo mashabiki wetu jamani tu-relax.” Kaongeza.