Baresi agomea likizo nyota wake

Summary

  • Prisons iliwapa mapumziko mafupi nyota ya takribani siku tano tangu walipomaliza mchezo wao dhidi ya Namungo walioshinda mabao 3-2 na leo wanarejea tena mzigoni kujiwinda na mechi zinazofuata.

MBEYA. WAKATI Tanzania Prisons ikirejea mazoezini leo Jumatatu, kocha mkuu wa timu hiyo Abdalah Mohamed ‘Baresi’ amesema ameamua kuwawahisha nyota wake kambini kutokana na matokeo waliyonayo.

Prisons iliwapa mapumziko mafupi nyota ya takribani siku tano tangu walipomaliza mchezo wao dhidi ya Namungo walioshinda mabao 3-2 na leo wanarejea tena mzigoni kujiwinda na mechi zinazofuata.

Timu hiyo hadi sasa ipo nafasi ya 14 kwa pointi 25, inatarajia kushuka uwanjani Aprili 16 kuwavaa maafande wenzao, Ruvu Shooting walioshinda dhidi ya Mbeya City 2-1 na kukaa nafasi ya 15 kwa pointi 20.

Baresi aliliambia Mwanaspoti kuwa wangeweza kupumzika hata zaidi ya wiki mbili, lakini kutokana na matokeo waliyonayo imewafanya kuwahi kambini kuendelea na mazoezi kujiandaa na michezo iliyobaki.

Alisema pamoja na ushindi walioupata kwenye mechi iliyopita, lakini bado yapo makosa madogo kikosini ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ili michezo mitano iliyobaki waweze kushinda na kubaki salama ligi kuu.

“Ukiangalia matokeo yetu utagundua tunahitaji muda wa kutosha kujisahihisha ili tujikwamue nafasi za mkiani, sisi hatuna likizo ya kula bata, tuna mechi ngumu ambazo tunataka pointi ili kubaki salama ligi kuu,” alisema Baresi.

Kocha huyo aliongeza kuwa kwa sasa hawajiandai na mchezo mmoja dhidi ya Ruvu Shooting bali michezo yote waliyonayo ni hesabu kubwa ya kushinda zote huku akichekelea kiwango walichoonesha nyota wake dhidi ya Namungo.

“Mchezo ujao ni dhidi ya Ruvu Shooting, lakini sisi tunafikiria michezo mitano tunatoboaje ili kufikia malengo, nilikoshwa na makali ya straika kwenye mechi iliyopita lazima twende kwa kasi hiyo,” alisema kocha huyo.