Bares na mitihani minne Prisons

Muktasari:

  • Bares anatua kwenye kikosi hicho kikiwa na mwenendo mbovu huku mabosi wakiwa na presha ya kuiona timu hiyo inasalia Ligi Kuu Bara.

MBEYA. KOCHA mpya wa Tanzania Prisons, Mohamed Abdalah 'Bares' yupo viunga vya Jiji la Mbeya tayari kwa kuanza majukumu mapya na Wajelajela hao ambao Ijumaa watakipiga na Mtibwa Sugar, Uwanja wa Sokoine kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Bares anatua kwenye kikosi hicho kikiwa na mwenendo mbovu huku mabosi wakiwa na presha ya kuiona timu hiyo inasalia Ligi Kuu Bara.

Kocha huyo anakabiliwa na mitihani minne ndani ya Prisons, mojawapo ni kuhakikishan timu inasalia Ligi Kuu Bara licha ya kibarua kigumu iliyokuwa nayo.
Prisons inakabiliwa na michezo mitano ugenini kati ya tisa iliyosalia kufunga msimu na minne ya nyumbani ni dhidi ya Mtibwa, Ruvu Shooting, KMC na Yanga.
Mtihani wa tatu inakutana na timu ambazo zipo kwenye hatari ya kushuka daraja kama vile Polisi Tanzania, Ruvu Shooting pamoja na Coastal Union.

Pia wapinzani wake wananufaika kwa kuwa kwenye viwanja vya nyumbani huku Yanga inayosaka kutetea ubingwa itacheza nayo Uwanja wa Sokoine, mchezo wa kufunga msimu.

Mbaya kwa Prisons ni Yanga haitakuwa tayari kumaliza msimu kwa kichapo pia haitakuwa tayari kupoteza tena kwenye ardhi ya Mbeya baada ya kuharibiwa 'unbeaten' yao na Ihefu Novemba 29 kwa kufungwa 2-1.

Bares mtihani mwingine ni kurejesha morali sio tu kwa wachezaji bali hata mashabiki ambao walionekana kukata tamaa kwani hata mchezo wa mwisho dhidi ya Ihefu hawakutokea wengi uwanjani.

Katibu Mkuu wa timu hiyo, Ajabu Kifukwe alisema makocha sita waliomba kazi, watatu wazawa na watatu kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Ghana na Cameroon lakini wao wakampitisha Bares.

Bares ambaye hivi karibuni alichukua ubingwa wa Kombe la Mapinduzi akiwa na Mlandege anachukua nafasi ya Patrick Odhiambo aliyefungashiwa virago saa chache baada ya kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Ihefu ikiwa nyumbani.

Bares amewahi kuifundisha timu hiyo misimu wa mwaka 2022/21 kisha akatimka JKT Tanzania na baadaye akatimkia Zanzibar kujiunga na Mandege.