Barbara: Utamu unakuja Simba

Monday August 02 2021
barba pic
By Thobias Sebastian

WAKATI Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes akipitisha usajili wa Mmalawi, Peter Banda, Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez amesema mambo matamu zaidi yanakuja Msimbazi chini na bilionea na Mwekezaji wao, Mohammed ‘Mo’ Dewji.

Barbara alisema mafanikio iliyopata Simba msimu huu imetokana na uwekezaji wa Mo Dewji, lakini kuna makubwa zaidi yanakuja baada ya bilionea huyo na Mwenyekiti wa Bodi ya klabu hiyo kuahidi kuweka mkwanja zaidi ili kuimarisha timu yao na kuhakikisha wanabeba ubingwa wa Afrika.

Alisema moja na eneo walilolipania ni usajili wa wachezaji na maandalizi ya kishindo kwa ajili ya msimu ujao ili kuvuka pale walipoishia kwa msimu huu.

barba pic 1

“Tunakwenda kuwekeza zaidi kwa upande wa wachezaji ili kuwa nao bora ndani ya kikosi na inshallah mambo mazuri yataonekana katika mashindano hayo,” alisema Barbara na kuongeza;

“Katika kipindi cha usajili mambo mazuri yataonekana katika eneo hilo kwa kupata wachezaji bora kulingana na mapungufu yetu ambayo yalionekana msimu huu.”

Advertisement

Juzi kwenye mkutano wake na waandishi akikabidhi cheki ya Sh 20 bilioni, Mo Dewji alisema Simba ijayo inalitaka taji la Afrika na kuahidi kufanya usajili wa kishindo, huku akiwa amempa mkataba mpya Kocha Gomes ili aendelee kumwaga maujuzi yake Msimbazi. Mo Dewji alisema katika miaka minne aliyoiongoza Simba kubeba ubingwa wa Ligi Kuu kwa msimu minne, alikuwa akitumia kila mwaka zaidi ya Sh 5 bilioni, lakini msimu ujao dau litaongezwa ili mambo yawe bulbul na Barbara akakazia hapo kwa kusema kwa mikakati waliyoiandaa wapinzani wao iwe katika Ligi Kuu Bara na CAF wajipange kwelikweli kwa mziki utakuwa moto zaidi.

Hadi sasa tayari wachezaji wanne wa kizawa wameshanaswa na Simba tayari kwa msimu ujao, huku wengine wakiendelea kujadiliwa wakiwamo nyota wa kigeni.

Nyota hao wapya na wale waliokuwapo msimu uliopit, Agosti 10 watakwea pipa kuelekea katika mji wa kitajiri Alexandria Misri kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao (Pre Season).

Kikosi hicho cha Simba wakiwa hapo Alexandria kwa wiki mbili mbali ya kufanya mazoezi mbalimbali magumu watacheza mechi za kirafiki na baadhi ya timu za nchini humu ambazo zitakuwa na nafasi.

Mwanaspoti limepata taarifa kutoka ndani ya Simba wachezaji wote wa timu hiyo wameshatuma hati zao za kusafiria (Passport), na zipo katika ubalozi wa Egpty kwa ajili ya kupata visa za kuingia nchini humo.

Advertisement