Baobab Queens yapiga ligi kusimama

Muktasari:

Ligi Kuu ya Wanawake imesimama kupisha maandalizi ya timu ya taifa Twiga Stars

Dodoma. Uongozi wa timu ya Baobab Queens ya Dodoma umesema kusimamishwa kwa Ligi Kkuu ya Wanawake Bara baada ya kuchezwa mechi nne ni kuziongezea timu mzigo wa gharama.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa juzi baada ya kumalizika kwa raundi ya nne ya ligi hiyo sasa itaendelea mwezi ujao kupisha maandalizi ya timu ya taifa ya wanawake Twiga Stars itakayokuwa kambini kujiandaa na mechi zake za kimataifa.

Kocha Baobab Queens, Mwambegele Kakolanya alisema kusimama kwa ligi yao ni pigo kwa timu yake inawaongezea ghalama.

 “Kiukweli nasikitika kusogezwa kwa ligi yetu hii ni taarifa mbaya kwetu kwani kutatuongezea ugumu zaidi wa kukabiliana na ukata kwa sababu kwa wakati huu mambo ni magumu itakuwaje kukaa na wachezaji mwezi mzima wakisubiri kambi ya timu ya taifa ivunjwe?”.Alihoji Kakolanya

Hoja ya kocha huyo inakuja baada ya awali Mwenyekiti wa timu hiyo Innocensia Massawe kulalamikia kusogezwa mbele kwa ligi hiyo.

“Kuweka wachezaji kambini mwezi mzima inahitaji gharama,  pia ukisema uvunje kambi ni gharama nauli za kuwarudisha makwao na kuwarudisha kambini tena ili ligi iendelee zitatoka wapi,” alisema Massawe

Hadi ligi inasimama timu ya JKT Queens inaongoza ikiwa na pointi 12 , ikifuatiwa na Sisterz Kigoma yenye pointi 9, Alliance Girls (7), Mlandizi Queens (6), Baobab Queens (5), Simba Queens (3), Panama (2) na Evergreen Queens (1).