Baleke mambo bado kabisaaa

Muktasari:

  • Hadi sasa Baleke anamiliki mabao matano kwenye Ligi Kuu Bara na mawili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, jambo alilosema halitoshi, badala yake anataka kufanya vitu vikubwa zaidi ili mradi tu wanafikie malengo.

STRAIKA wa Simba, Jean Baleke amesema ana kazi kubwa ya kuifanya  ili kuhakikisha huduma yake inakuwa na manufaa ndani ya kikosi hicho na mashabiki wanafurahia burudani anayoitoa anapokuwepo uwanjani.

Hadi sasa Baleke anamiliki mabao matano kwenye Ligi Kuu Bara na mawili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, jambo alilosema halitoshi, badala yake anataka kufanya vitu vikubwa zaidi ili mradi tu wanafikie malengo.

Nyota huyo alisema kwamba Simba ni klabu kubwa inahitaji wachezaji wanaofanya mambo makubwa zaidi, hivyo anaendelea kujipanga siku hadi siku ili huduma yake iendelee kutegemewa ndani ya timu.

“Kwa nafasi yangu ninayocheza ina ushindani mkali na kila mchezaji anapambana kuisaidia timu. Ndio maana nasisitiza nina kazi kubwa ya kufanya niwe sehemu ya wachezaji wanaotambulika kwa kiwango bora,” alisema Baleke

“Ingawa siyo kazi ndogo kufunga mabao matano kwenye mechi mfululizo, hiyo inanipa nguvu kwamba kila penye dhamira na bidii hakuna kinachoshindikana.”

Baleke ambaye ni kati ya wachezaji wanne ndani ya kikosi cha Simba wanaomiliki hat-trick, alisema uwepo wa hat-trick hizo unaonyesha namna ambavyo wachezaji wanatambua timu inahitaji nini kutoka kwao.

“Hat trick hizo ni kati ya ishara zinazoonyesha Simba inahitaji vitu vikubwa  ambavyo vinatakiwa vifanywa na sisi wachezaji kwa umoja wetu, kwani wote tupo kwa ajili ya kujenga timu na sio vingine,” alisema.

Hatrick hizo kiungo Clatous Chama alifunga dhidi ya Horaya mechi ya makundi ya CAF Simba ikishinda (7-0), nahodha John Bocco dhidi ya Ruvu Shooting, Saido dhidi ya Prisons na Baleke dhidi Mtibwa Sugar.