Baleke, Kanoute nao wachomoza

Muktasari:

  • Chama na Lipelo kila mmoja amefunga mabao manne kwa sasa katika raundi ya tano ya makundi ya michuano hiyo, iliyosaliwa na mechi za raundi ya mwisho zitakazopigwa Aprili Mosi zitakazoamua timu za kwenda robo fainali kuungana na Raja Casablanca ya Morocco, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Esperance ya Tunisia zilizotangulia mapema.

MABAO mawili mawili yaliyofungwa na Jean Baleke na Sadio Kanoute wa Simba yamewaingia kwenye anga za mastaa wengine wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika orodha ya wafungaji wanaoongozwa kwa pamoja na Clatous Chama wa Simba na Makadi Lipelo wa Al Hilal.

Chama na Lipelo kila mmoja amefunga mabao manne kwa sasa katika raundi ya tano ya makundi ya michuano hiyo, iliyosaliwa na mechi za raundi ya mwisho zitakazopigwa Aprili Mosi zitakazoamua timu za kwenda robo fainali kuungana na Raja Casablanca ya Morocco, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Esperance ya Tunisia zilizotangulia mapema.

Baleke aliyesajiliwa dirisha dogo na Kanoute walifunga mabao yao wakati Simba ikiizamisha Horoya ya Guinea katika mechi ya Kundi C kwa mabao 7-0, huku Chama akipiga hat-trick na kumfanya apae hadi kileleni mwa orodha ya wafungaji, akiwapiku wachezaji wengine waliokuwa juu yake hapo awali.

Wachezaji wanaofuata kwenye orodha ya mabao hadi sasa ni  Hamza Khabba wa Raja, Cassius Mailula na Peter Shalulile wa Mamelodi pamoja na Kahraba wa Al Ahly wenye mabao matatu kila mmoja, huku Baleke na Kanoute wakifuata sambamba na wachezaji wengine 10 wenye mabao mawili kila akiwamo Percy Tau na Mohamed Sherif (Al Ahly) na Ben Hammouda (Esperance).

Wengine wenye mabao mawili mawili ni;  Soufiane Banjdida na Walid Sabbar (Raja), Khuliso Mudau (Mamelodi), Pape Ndiaye (Horoya), Paul Sergio (Al Merrikh), Leonel Wamba (CR Belouizdad) na Patient Wassou (CotonSport), huku jumla ya mabao 85 yakiwa yamefungwa hadi sasa katika makundi.

Katika mechi tano ilizocheza Simba, imefunga jumla ya mabao saba na kuruhusu manne langoni mwao na Aprili Mosi itaikabili Raja mjini Casablanca ikikumbukwa kufungwa mabao 3-0 nyumbani.