Baba Kanumba afungua moyo kwa Lulu

Muktasari:
Akizungumza na MCL Digital leo Ijumaa, Mzee Kusekwa ameshauri mamlaka zinazohusika kumwachia huru Lulu kama inawezekana kwani adhabu aliyotumikia inatosha.
Siku 6 baada ya msanii wa Bongo Movie, Elizabeth Michael 'Lulu' kuachiwa huru na kutumikia kifungo cha nje, baba wa marehemu Steven Kanumba, Charles Kusekwa amesema uamuzi wa kubadirishiwa adhabu kwa msanii huyo ni sahihi.
Akizungumza na MCL Digital leo Ijumaa, Mzee Kusekwa ameshauri mamlaka zinazohusika kumwachia huru Lulu kama inawezekana kwani adhabu aliyotumikia inatosha.
"Unajua kila mtu anamawazo yake, mimi naona ni sawa tu kubadirishiwa adhabu kwa Lulu, maana bado Jela ni ileile na sio kama kaachiwa huru, na hata kama ingewezekana ningeiomba mamlaka husika wangemwachia tu huru, maana haya mambo ni mipango ya Mungu, na kutokana na ushahidi wake Jaji ameona hakukusudia kufanya hivyo, kwa hiyo hakufanya makusudi huyu mtoto na ameshajuta kwa kitendo alichokifanya maana si kwa kudhamiria,"anasema Mzee Kusekwa.
"Pia, namshauri mzazi mwenzangu, Mama Kanumba, najua ameumia ila angeachana na mambo hayo asilalamike, cha msingi ni kumwombea kwa Mungu mtoto wetu kwani huyu binti (Lulu) amejuta na kujifunza."
Maneno haya ameyatoa Mzee Kusekwa yanapisha na yale ya Mama Kanumba ambaye baada ya kusikia Lulu amepewa adhabu ya kutumikia kifungo cha nje ni kama hakuridhika.