Baba Bacca atoa siri ya Yanga

Muktasari:

  • Baba huyo anafahamika kwa jina la Abdallah Hamad, ameliambia Mwanaspoti kuwa, mbinu za Kocha Miguel Gamondi ndizo zitakazoendelea kuipoteza Yanga na kutoka na ushindi japo hafikirii kama zile tano zitajitokeza tena Kwa Mkapa kesho Jumamosi.

IKIWA imesalia saa chache kabla ya mtanange wa Kariakoo Dabi, baba mzazi wa beki wa Jangwani, Ibrahim Bacca amebashiria Yanga kuibuka na ushindi kwa mara nyingine mbele ya Simba, huku akiweka bayana kitakachoibeba timu hiyo anayoishabikia anayoichezea mwanae.

Baba huyo anafahamika kwa jina la Abdallah Hamad, ameliambia Mwanaspoti kuwa, mbinu za Kocha Miguel Gamondi ndizo zitakazoendelea kuipoteza Yanga na kutoka na ushindi japo hafikirii kama zile tano zitajitokeza tena Kwa Mkapa kesho Jumamosi.

Akizungumza akiwa visiwani Zanzibar, Baba Bacca  amesema kitu kingine kutakaibeba Yanga kuibuka na ushindi sio kwa sababu ya ubora wa wachezaji bali ni mbinu hatari zinazozitesan timu nyingine msimu huu mbele ya vinara hao wa Ligi Kuu Bara.

"Yanga inacheza kwa kujituma sana dakika 90, hawachoki tofauti na wapinzani, jambo ambalo ni hatari sana kwani kikosi cha namna hiyo kinaweza kukufunga," amesema baba Bacca na kuongeza;

"Ukiachana na ubora wa kina Azizi Ki, Pacome, Diarra, Bacca na wengine, timu hii ina mawasiliano mazuri ndio maana hawapotezi nafasi nyingi au kufungwa sana, kulinganisha na wapinzani wao kwa msimu huu chini ya Gamondi. Kwa Jumamosi (kesho) mtani ana kazi ya ziada kwani anatakiwa kujitafuta katika maeneo mengi ili kuwa bora zaidi anapokutana na Yanga."

Hata hivyo, Baba Bacca ameonya Yanga haipaswi kuingia uwanjani kwa kujiamini kuopita kiasi kwani Dabi huwa na matokeo ya kushangaza hasa kwa timu inayochukuliwa poa kupindua meza, hivyo Chama lake liingie uwanjani likiiheshimu Simba, lakini ikipambana kutimiza malengo ya kuzoa pointi zote tatu.

Yanga walio wenyeji wa pambano hilio la marudiano la Ligi Kuu Bara, itavaana na Simba ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 5-1 iliyopata mechi ya kwanza ya Novemba 5, mwaka jana, lakini ikiwa nafasi nzuri katika msimamo ikikusanya pointi 55 kupitia mechi 21, huku Simba ikiwa ya tatu na pointi 46 kwa mechi 20.