Aziz Ki: Nakuja Yanga, asisitiza Yacouba asiachwe
WAKATI wadau wakishangazwa na uongozi wa Yanga, kumbakiza mshambuliaji wao majeraha Yacouba Sogne, imefichuka siri nyuma ya pazia iliyowalazimu kufanya hivyo.
Mwanaspoti limepenyeza za uhakika za ndaani kabisa kwamba Staa wa Asec Mimosas, Stephane Aziz Ki, raia wa Burkina Faso ambaye amewaambia anataka kucheza na Yacouba na kama wakimtema haji anaenda zake Zamalek ya Misri.
Yanga walivutika na kiwango alichokuonyesha Aziz Ki kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, akifunga mabao matatu, hivyo Nasreddine Nabi kumuona kama mtu sahihi wa kutetea heshima ya Yanga kimataifa.
Habari za uhakika zinasema kwamba Aziz Ki yupo tayari kukipiga Jangwani kwa sharti la kumuongezea mkataba Yacouba.
“Ni kweli Yanga imepeleka ofa kwa Aziz Ki kati ya masharti aliyowapa ni kumpa mkataba rafiki yake Yacouba, akiwasisitiza wakifanya hivyo atakuwa tayari kuwatumikia msimu ujao na hatakwenda Simba wala Zamalek,” kilisema chanzo hicho.
“Ni suala la muda tu mchezaji huyo kumalizana na Yanga kwasababu masharti ambayo ameyatoa yameanza kufanyiwa kazi ikiwemo mshahara ambao umechangamka kidogo, hivyo muda wowote kuanzia sasa Yacouba anaweza akasainishwa mkataba mpya,”kilisema chanzo chetu ingawa mpango wa Yanga ilikuwa kumtoa Yacouba kwa mkopo Singida Stars.
Chanzo hicho kilieleza lengo la kumsajili Aziz Ki ni kumuongezea nguvu Fiston Mayele kinara wa mabao 14 Ligi Kuu Bara.
Awali Mwanaspoti lilisharipoti kuwa Yacouba bado ataendelea kuitumika Yanga kwa kuongezewa mkataba kutokana na kuumia akiwa ndani ya timu na uongozi uligharamikia matibabu yake, kauli hiyo aliwahi kuitoa mjumbe wa kamati ya usajili wa timu hiyo, Hersi Said.
“Bado tuna mpango na Yacouba, tutamuongezea mkataba mpya, kwa sababu ametoka kwenye majeruhi atahitaki muda ili kurudi kwenye hari yake, kocha Nabi anataka mchezaji wa kuingia moja kwa moja kikosini itatubidi tumtoe kwa mkopo ili akarudishe uwezo wake,” alisema.