Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aziz KI, Lomalisa hesabu kali Sauzi

WAKATI Yanga ikiwa na siku mbili katika ardhi ya Afrika Kusini kujiandaa na mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns, mastaa wa timu hiyo wamefunguka kiu waliyonayo ya kuandika rekodi kwa kuipeleka Yanga nusu fainali ikiwa ugenini.

Yanga na Mamelodi zilitoshana nguvu katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyopigwa Jumamosi iliyopita Kwa Mkapa na keshokutwa (Ijumaa) zitarudiana katika pambano litakalopigwa jijini Pretoria kuanzia saa 3:00 usiku.

Yanga inahitaji sare yoyote ya mabao au ushindi ili kufuzu nusu fainali kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa na mastaa wa timu hiyo, Stephane Aziz KI na Joyce Lomalisa wamezungumzia mchezo huo na kusema wachezaji wana morali na kuipania mechi hiyo ya Ijumaa.

Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti, Aziz KI na Lomalisa walisema baada ya dakika 90 za nyumbani wametua Sauzi kwa nia moja tu ya kushinda ugenini.

Aziz amesema hawana presha yoyote na wenyeji licha ya kukiri ni timu ngumu na kubwa yenye mafanikio makubwa kwa miaka ya hivi karibuni, lakini hata Yanga ni timu bora na kiu ya kila mmoja kikosini ni kuona inasahihisha makosa yaliyowakwamisha kupata ushindi nyumbani.

Kiungo mshambuliaji huyo amesema katika mechi ya awali ya Kwa Mkapa hakuwa amepata muda mzuri wa maandalizi ya mchezo, ndio maana alijikuta anabanwa na misuli lakini mechi ya Ijumaa ana kesi ya kumalizana na Mamelodi japo anafahamu haitakuwa mechi rahisi kwa pande zote mbili.

"Mechi itakuwa ngumu lakini Yanga ina nafasi ya kufanya vizuri na kama tutapata matokeo basi yawe ya mapema kuwafanya wapinzani wawe na presha kubwa kutokana na matokeo ya mchezo uliopita, kurejea kwa wenzetu waliokuwa majeruhi ni faida kwa kikosi chetu na tutahakikisha tunawafurahisha mashabiki waliosafiri na wale ambao tumewakuta Afrika Kusini," amesema Aziz Ki na kuongeza;

"Hatuna presha tutacheza na Mamelodi tukiwa na malengo ya kutaka kufuzu, tumeshacheza nao tunawajua, tulipokuwa nyumbani tulifanya makosa ya kutotumia nafasi lakini ugenini tutafatuta bao au mabao ili kuwaweka kwenye presha wapinzani wetu."

Kwa upande wa Lomalisa amesema mechi haitakuwa rahisi lakini anaamini washambuliaji wa timu hiyo hawatafanya makosa mara mbili wataweza kupata bao kule ugenini ambalo litasaidia kurahisisha kazi kwa kikosi hicho kuandika historia Afrika.

"Morali yetu iko juu, naridhishwa na mazoezi yanayoendelea ambayo yalikuwa ya kwanza tangu tufike hapa na ninaamini kama tutapata bao la mapema hiyo itakuwa kama kitanzi kwa safu ya Mamelodi," alisema Lomalisa.