Aziz KI, Himid wawahishwa hospitali
Muktasari:
- Hiyo ilikuwa katika mechi ya Kundi B katika Kombe la Shirikisho Afrika iliyochezwa leo Novemba 28, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar na Wydad kushinda 1-0.
Kiungo mshambuliaji wa Wydad Athletic, Stephanie Aziz KI na Himid Mao wa Azam, wamelazimika kuwahishwa hospitali kwa dharura baada ya kuumia kwenye mechi baina ya timu hizo.
Hiyo ilikuwa katika mechi ya Kundi B katika Kombe la Shirikisho Afrika iliyochezwa leo Novemba 28, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar na Wydad kushinda 1-0.
Viungo hao waligongana wakati wanawania mpira dakika ya 74, kisha kufanyiwa mabadiliko ambapo Azizi KI nafasi yake ilichukuliwa na Mohammed Rahyi wakati Himid akiingia Yahya Zayd.
Viungo hao walitolewa kwa vitanda vya wagonjwa baada ya tukio hilo wakipelekwa moja kwa moja vyumbani wakiwa na madaktari wa timu zao.
Hata hivyo, wakati mechi inaendelea, wachezaji hao walilazimika kuwahishwa hospitali kwa magari maalum ya wagonjwa wa dharura.
Bado haijajulikana ni wapi wachezaji hao wameumia zaidi baada ya tukio hilo huku wakiibua presha kwa timu zao.
Wakati Aziz KI akitolewa, familia ya mke wake ikiongozwa na mama mkwe wake, Mama Mobetto, ilikuwa jukwaani ikionekana kuwa na presha.