Azam bado hali tete, yapoteza mechi ya pili CAF
Muktasari:
- Licha ya kupoteza mechi hiyo ya Kundi B katika Kombe la Shirikisho Afrika, Azam ilianza vizuri kipindi cha kwanza ikicheza kwa tahadhari kubwa huku ikishambulia kwa hesabu kali.
AZAM FC ikicheza nyumbani Uwanja wa Amaan kisiwani Zanzibar, imepokea kipigo cha pili leo Novemba 28, 2025 baada ya kufungwa bao 1-0 dhidi Wydad Athletic ya Morocco.
Licha ya kupoteza mechi hiyo ya Kundi B katika Kombe la Shirikisho Afrika, Azam ilianza vizuri kipindi cha kwanza ikicheza kwa tahadhari kubwa huku ikishambulia kwa hesabu kali.
Wydad ilianza kutengeneza nafasi nzuri dakika ya pili, Stephanie Aziz KI alipokaribia kuifunga Azam, lakini hesabu zake za kuinua mpira zilifeli, kipa Zuberi Foba akapangua shambulizi hilo na kuwa kona.
Azam ilifanikiwa kuweka mpira wavuni dakika ya sita kupitia mshambuliaji wake Jephte Kitambala kwa shambulizi la kona lakini mwamuzi alilikataa akidai kulikuwa na kusukumana kabla ya kufungwa kwa bao hilo.
Azam ilitengeneza nafasi nzuri dakika ya 15, Feisal Salum alishindwa kumalizia.
Idd Seleman 'Nado' alipoteza nafasi nyingine nzuri kwa Azam akiwa karibu na eneo la hatari shuti lake likapaa wakati wenzake wakisubiri kupewa pasi wakiwa eneo zuri.
Majukwaani mashabiki wa soka walikuwa wengi wakiishangilia Azam FC baada ya wadhamini wa klabu hiyo kununua tiketi zote za mechi hiyo.
Kundi kubwa la mashabiki wa Wydad nao walikuwa jukwaani wakiishangilia kwa nguvu timu yao wakiwa na mavazi ya jezi nyekundu.
Kitambala tena akapata nafasi nyingine akishindwa kuitumia dakika ya 27, shuti lake hafifu lilidakwa kirahisi na kipa El Mehdi Benabid.
Mpaka mapumziko timu hizo zilitoka bila kufungana huku Azam ikiwabana vizuri wageni wao, Wydad.
Kipindi cha pili Wydad walikianza kwa mabadiliko wakimtoa Benjamin Bouchouri nafasi yake ikichukuliwa na Mohammed Moufid.
Wydad iliendelea kumiliki mpira na kufanikiwa kupata bao kupitia Nordin Amrabat dakika ya 57 kwa shuti la mguu wa kushoto akipokea pasi ya nyuma ya Thembinkosi Lorch.
Azam iliamka baada ya kuruhusu bao hilo lakini bado haikuwa na nguvu kuilazimisha Wydad kufanya makosa kwenye ukuta wao.
Kitambala alipoteza nafasi ya kufunga kwa kichwa dakika ya 78 kupitia mpira wa kona ya Fei Toto.
Katika mechi hiyo, Wydad baada ya mabadiliko ya kwanza dakika ya 45, baadaye dakika 76 ikamuingiza Mohamed Elowasti na kumtoa Thembinkosi Lorch, dakika ya 80 kiungo Stephane Aziz Ki akatolewa na kuingia Rayhi, kisha ikamaliza dakika 88 kwa kumtoa Hamza Hannouri na kumuingiza Tumosang Orebonye.
Azam ilimtoa Himid Mao na kumuingiza Yahya Zayd, yakiwa ni mabadiliko pekee yaliyofanywa na Kocha Florent Ibenge.
Mpaka mwisho wa mechi hiyo, Azam imetoka vichwa chini kwa kupoteza kwa mara nyingine katika Kundi B, baada ya wikiendi iliyopita kuchapwa mabao 2-0 na AS Maniema nchini DR Congo.
VIKOSI
AZAM: Zuberi Foba, Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Yoro Diaby, Fuentes Mendoza, Himid Mao/Yahya Zayd, Abdul Seleman 'Sopu', Sadio Kanoute, Jephte Kitambala, Feisal Salum 'Fei Toto', Idd Seleman 'Nado'
WYDAD: El Mehdi Benabid, Benjamin Bouchouri/Mohammed Moufid, Giilherme Fereira, Amine Aboulfath, Ayoub Boucheta, Joseph Bakasu, Walid Sabbar, Stephanie Aziz KI, Nordin Amrabat, Thembinkosi Lorch/Hamza Elowast, Hamza Hannouri.