Aziz Ki, Guede wamtisha kocha

Muktasari:

  • Nawina pia ameukubali mziki wa Yanga akikiri kuwa ubora walionao wachezaji wake ndiyo uliowapa tabu na kukubali kichapo cha mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, juzi.

KOCHA Msaidizi wa Singida Fountain Gate, Ngawina Ngawina ameshtushwa na viwango vya wachezaji wa Yanga, Aziz KI na Joseph Guede kutokana na namna wanavyoendelea kuviboresha na kuwa wazuri zaidi uwanjani.

Nawina pia ameukubali mziki wa Yanga akikiri kuwa ubora walionao wachezaji wake ndiyo uliowapa tabu na kukubali kichapo cha mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, juzi.

Akiiongoza Singida Fountain Gate juzi katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza, ilikumbana na kichapo hicho licha ya uwanja kujaa maji, lakini mastaa wa Yanga hawakupata tabu yoyote.

Katika mchezo huo ambao ulikuwa na upinzani mkali, mabao ya Joseph Guede aliyetupia mawili na Stephen Aziz Ki yalitosha kuwalaza wapinzani hao na kubaki kileleni kwa pointi 55.

Ngawina amesema licha ya kupoteza kwa Yanga siyo mwisho wa safari kwani bado wana nafasi ya kufanya vizuri michezo saba ya mwisho iliyobaki na kutimiza malengo ya kutoshuka daraja.

“Tumepoteza mchezo na tunaheshimu matokeo tulifanya makosa Yanga wakayatumia kutuadhibu, lakini vijana walicheza vizuri japokuwa hatukufikia malengo,” amesema.

“Tunakwenda kujiandaa mchezo unaofuata dhidi ya Ihefu kuhakikisha tunasahihisha makosa na kufanya vizuri ili kufikia malengo yetu ya kubaki kwenye ligi.”

Kocha huyo ameongeza kuwa benchi la ufundi linakwenda kuisuka timu kwa kuongeza makali maeneo ya straika na beki kuhakikisha michezo iliyobaki hawaachi kitu.