Aziz KI ana jambo lake, apania kuweka rekodi

Aziz Ki afunguka mazito, asema kazi aliyopewa Yanga

KIKOSI cha Yanga kinaendelea kujifua kambini Avic Town, Kigamboni kwa maandalizi ya mechi zao zijazo, lakini mmoja wa nyota wa timu hiyo, Stephane Aziz Ki ametamba kuwa, amejipanga kufanya mambo makubwa msimu huu katika michuano ya CAF ili kuona Yanga inatoboa makundi.

Aziz Ki alisema licha ya Yanga kurudi uwanjani wikiendi hii kuvaana na Ruvu Shooting, lakini akili ya kila mchezaji wa kikosi hicho ni mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan, huku akipania kufanya makubwa kuendeleza rekodi alizonazo katika michuano hiyo.

Msimu uliopita akiwa na ASEC Mimosas kabla ya kusajiliwa na Yanga msimu huu, Aziz Ki alitinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na kukwama kwenda robo fainali baada ya timu hiyo ya Ivory Coast kuzidiwa ujanja na RS Berkane ya Morocco iliyotwaa taji na Simba waliokuwa kundi moja.

Akizungumza na Mwanaspoti, Aziz KI alisema juu ya uchu alionao kwa mechi hizo za kuamua kutinga makundi dhidi ya Al Hilal, akisisitiza hataki masihara kwenye mechi za kimataifa kwani ndizo zilizomleta Yanga na yupo tayari kuendelea alipoishia.

Nyota huyo kutoka Burkina Faso alisema anajivunia kuwa Yanga kwani ni klabu kubwa na anaamini itafanya vizuri mbele ya Al Hilal, licha ya kukiri ni timu ngumu kwa vile wachezaji wote wameweka nguvu ili kutoboa na kutinga makundi, ikiwa ni mara ya kwanza tangu ilipofanya hivyo mwaka 1998.

“Yanga iliniona kupitia michuano ya CAF nikiwa na Asec, nikiwa kule nilifanya nililoliweza na sasa nipo Yanga nitahakikisha nakuwa bora zaidi, nataka kuendeleza rekodi kwa manufaa ya timu hii. Nina uzoefu kwa sasa na sitaki kufanya makosa pale nitakapopata nafasi, naamini kwa kushirikiana na wenzangu tutafanya vizuri zaidi,” alisema Aziz Ki aliyerejea kutoka kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Burkina Faso.

Akiwa na Asec aliisaidia kuipa taji la 28 la Ligi Kuu ya Ivory Coast kama ilivyo kwa Yanga na amewaita mashabiki Kwa Mkapa katika mechi ya mkondo wa kwanza itakayopigwa Oktoba 8 kabla ya kuwafuata Hilal kwao kwa mchezo wa marudiano utakaochezwa Oktoba 16.