Aziz KI ampindua Fei Toto, afikia rekodi ya Mayele

Muktasari:

  •  Dodoma Jiji haijawahi kuifunga Yanga tangu zilipoanza kukutana kwani mara ya mwisho kabla ya mchezo huu zilikutana hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ambapo ilichapwa mabao 2-0, Uwanja wa Jamhuri Aprili 10, mwaka huu.

MABAO mawili aliyofunga kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki katika ushindi wa wa 4-0 dhidi ya Dodoma Jiji yamemfanya kufikisha 17, hivyo kuwa kinara akimpiku nyota wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto' mwenye 16.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Aziz Ki amefunga mabao hayo dakika ya 45 kwa mkwaju wa penalti baada ya kuangushwa eneo la hatari na beki wa Dodoma, Augustino Nsata kisha kutupia la pili dakika ya 51.

Yanga ambao tayari imetangaza ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu kwa mara ya tatu mfululizo na wa 30 kwa ujumla tangu 1965, ilianza kupata bao la mapema katika dakika ya tisa kupitia kwa Clement Mzize anayefikisha mabao sita hadi sasa.

Wakati Dodoma Jiji ikipambana kushambulia ili kurejesha mabao hayo ilijikuta ikifungwa bao la nne katika dakika ya 78 ya mchezo huo lililofungwa na kiungo mshambuliaji wa kikosi hicho, Maxi Nzengeli anayefikisha mabao 10 msimu huu wa Ligi Kuu Bara.

Mabao mawili ya Aziz Ki yanamfanya kuifikia rekodi iliyowekwa msimu uliopita na aliyekuwa mshambuliaji nyota wa kikosi hicho Mkongomani, Fiston Mayele aliyemaliza mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akiwa amefunga 17 kisha kuondoka katika timu hiyo.

Msimu uliopita Mayele alifunga idadi hiyo sawa na kiungo mshambuliaji wa Simba Mrundi, Saidi Ntibazonkiza 'Saido' ambao wote walifungana hivyo kiwango kizuri alichokionyesha ndicho kilichowavutia mabosi wa Pyramids FC ya Misri waliomsajili.

Tangu Dodoma Jiji ipande Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/2020, imekutana na Yanga mara nane ambapo kati ya hizo haijawahi kushinda.

Tangu zilipoanza kukutana katika Ligi Kuu Bara ni mchezo mmoja tu kati ya minane ambayo hazijafungana ila mingine yote mabao yamefungwa.

Mchezo ulioisha bila bao kwa maana ya kushindwa kufungana baina ya timu hizi ulipigwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma, Julai 18, 2021. 

Katika michezo minane ya Ligi Kuu Bara timu hizo zilipokutana Yanga imekuwa mbabe zaidi kwani imefunga jumla ya mabao 20 wakati Dodoma imefunga matatu tu huku mechi iliyozalisha mabao mengi ni ile ya ushindi wa Yanga wa 4-2, Mei 13, mwaka jana.

Kwa maana hiyo Dodoma Jiji haijawahi kuifunga Yanga tangu zilipoanza kukutana kwani mara ya mwisho kabla ya mchezo huu zilikutana hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ambapo ilichapwa mabao 2-0, Uwanja wa Jamhuri Aprili 10, mwaka huu.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Aziz Ki amesema amefurahi kufunga mabao mawili na kuongoza katika vita ya ufungaji bora huku akiweka wazi jambo la kwanza na la msingi kwake ni kuhakikisha timu hiyo inapata matokeo chanya kwani ndio kitu cha msingi.

"Feisal ni rafiki yangu na napenda kile anachokifanya, kwangu naamini nitazidi kufunga zaidi ya hapa kwa sababu shauku yangu kubwa ni kuibuka mfungaji bora, ila yote kwa yote jambo kubwa ni kuona timu inaendelea kupata ushindi," amesema.