Prime
Aziz Ki afunguka ishu ya Mokwena

UNAKUMBUKA baada ya dakika 90 za mchezo wa Yanga na Mamelodi Sundowns pale kwa Mkapa kiungo Stephane Aziz Ki na kocha wa Mamelodi, Rulani Mokwena walionekana wakizungumza?
Haikuishia hapo, baada ya matuta kupigwa na mechi kuisha pale Loftus Versfeld, Sauzi, wawili hao walionekana wakipiga stori tena hadi pale kocha msaidizi wa Yanga, Moussa N’Daw alipowatenganisha kwa nguvu.
Mwanaspoti limepiga stori na Aziz Ki na kumuuliza mazungumzo yale mara mbili mfululizo walikuwa wanateta nini na nyota huyo akafafanua.
Aziz Ki alisema hususan kwenye mechi ya kwanza kauli ya Mokwena kwake ilikuwa ni kumwambia kuwa yeye ni mchezaji mzuri na ana kila sifa za kuwa mchezaji mkubwa huku akimtaka kubadilika kwenye eneo moja tu.
Alisema, Mokwena alimwambia kwamba anatakiwa kufanya uamuzi wa haraka kwenye maeneo hatari ili aweze kuwa bora zaidi eneo analocheza kwa kupachika mabao.
“Wewe ni mchezaji mkubwa unakila sifa una nguvu na unaumiliki mzuri wa mpira mguuni kwako ninakushauri uongeze uharaka eneo la umaliziaji ili kuweza kuwa bora kwa namba eneo unalocheza,” alisema Aziz Ki.
“Amenisisitiza kufanya hivyo akiamini kuwa pia naweza na nitakuwa bora zaidi kwa kuwa na namba nzuri ya ufungaji hili litalifanyia kazi na naamini nilianza kufanya hivyo mchezo wa marudiano ambapo nilifunga bao ambalo lilikataliwa,” alisema Aziz Ki ambaye ni kinara wa upachikaji mabao hadi sasa kwenye Ligi Kuu Bara akifunga mabao 13.
Pia alizungumzia mara nyingine alivyompa moyo nchini Afrika Kusini ambapo Yanga walitolewa kwa penalti 3-2 na bao lake kukataliwa, alisema baada ya mechi pia alimfuata na kumwambia amefanya alichomuelekeza.
“Alinipa moyo kuwa sitakiwi kukata tamaa kwa kile kilichotokea natakiwa kupambana zaidi ili kuonyesha ukubwa wangu, yaliyofanyika niyasahau nipambane zaidi huku akinipa sifa kuwa nimefanya alichokuwa amenielekeza,” alisema.
“Kaniambia kuwa uamuzi nilioufanya kwa kupata mpira eneo sahihi na kujaribu kupiga ni sahihi na natakiwa kuendelea kufanya hivyo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuipambania timu na kujiweka kwenye ubora kama mchezaji.”
Aziz Ki amefunga mabao 13 msimu huu sawa na kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Kwa mujibu wa mtandao wa Fotmob unaotoa takwimu mbalimbali za soka, Aziz KI msimu huu katika Ligi ya Mabingwa Afrika ametengeneza nafasi 18 za kufunga akiwa sambamba na kiungo nyota wa Simba, Mzambia Clatous Chama.
Idadi hiyo ni sawa na ya kiungo wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na raia wa Chile, Marcelo Allende aliyetengeneza pia 18. Nyota pekee aliyewazidi ni Mohamed Chibi wa Pyramids ya Misri na Ibrahima Keita wa TP Mazembe ambao kila mmoja ametengeneza 19.
Kwa upande wa kutengeneza nafasi kubwa za upatikanaji wa mabao, Aziz KI anaongoza pia akiwa nazo tano sawa na ilivyokuwa kwa Clatous Chama wa Simba waliofungana pia kwenye nafasi hiyo huku wakimpita Mohamed Chibi wa Pyramids aliyetengeneza nne.
Lakini taarifa zilizopo tayari amemalizana na Yanga kwa kuongeza mkataba wa miaka miwili na amekiri kuwa bado yupo yupo sana Jangwani.