Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Azam yavuta beki wa Ulaya

Muktasari:

  • Taarifa kutoka Afrika Kusini zinadai mazungumzo kati ya pande mbili zimekamilika na muda wowote kuanzia sasa nyota huyo atajiunga na Azam kwa ajili ya kuitumikia kwa msimu ujao wa 2026-2027.

AZAM FC inaendelea kuboresha kikosi kimya kimya kwa ajili ya msimu ujao na sasa imetua Ubelgiji kuinasa saini ya beki wa kati, Henri Braham Stanic anayecheza Stellenbosch FC ya Afrika Kusini.

Taarifa kutoka Afrika Kusini zinadai mazungumzo kati ya pande mbili zimekamilika na muda wowote kuanzia sasa nyota huyo atajiunga na Azam kwa ajili ya kuitumikia kwa msimu ujao wa 2026-2027.

Stanic aliyezaliwa Julai 18, 2002, katika manispaa ya Jette iliyoko Jiji la Brussels nchini Ubelgiji, alijiunga na Stellenbosch, Julai 15, 2025, akitokea Balzan FC ya Malta, ambapo mkataba wake ulikuwa unafikia ukomo rasmi kuanzia Juni 30, 2027.

Hata hivyo, licha ya kubakisha mkataba wa mwaka mmoja na Stellenbosch, taarifa zinadai uongozi wa Azam umefikia makubaliano ya kuipata saini yake na muda wowote atajiunga na timu hiyo inayofundishwa na Kocha Mkuu, Florent Ibenge.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu Msaidizi wa Azam, Rashid Seif alisema kinachoendelea kwa sasa katika timu hiyo ni mazungumzo na baadhi ya wachezaji mbalimbali kwa ajili ya kuwasajili na watakapokamilisha wataweka wazi rasmi majina yao.

Licha ya kucheza Stellenbosch FC na Balzan FC, Henri amecheza pia timu mbalimbali za vijana za RSC Anderlecht chini ya umri wa miaka 18, Oud-Heverlee Leuven chini ya miaka 23, zote za Ubelgiji, FK Jerv ya Norway na FK Liepaja ya Latvia.

Ujio wa nyota huyo, unaweka nafasi finyu ya beki wa kati wa timu hiyo, Yoro Mamadou Diaby ambaye taarifa zinadai huenda akaondoka, baada ya kukitumikia kikosi hicho kwa misimu miwili tangu aliposajiliwa akitokea Stade Malien ya kwao Mali.

Diaby alijiunga na Azam Julai 1, 2024, akitokea Stade Malien aliyocheza kwa mkopo kutoka akademi ya Yeleen Olympique ya kwao pia Mali, japo mustakabali wake na kikosi hicho kwa sasa uko shakani kutokana na ujio wa Mbelgiji huyo kutoka Stellenbosch.