Azam yagonga hodi rasmi Yanga na Sh400 milioni

Muktasari:

  • Moja ya klabu hizo ni Azam FC ambayo imegonga hodi Yanga kuulizia huduma ya mshambuliaji kinda, Clement Mzize.

Wakati msimu wa soka Tanzania ukiwa katika makumi yake ya mwisho, klabu kadhaa tayari zimeshaanza maandalizi ya msimu ujao.

Moja ya klabu hizo ni Azam FC ambayo imegonga hodi Yanga kuulizia huduma ya mshambuliaji, Clement Mzize kwa dau la Sh 400 milioni.

Azam FC ambayo inamalizia msimu bila kuwa na straika imepeleka ofa Yanga kutaka kumnunua mshambuliaji huyo ambaye mkataba wake na mabingwa hao wa kihistoria utaisha Juni 2025.

Tayari ofa iko mezani kwa Yanga na mambo yanakwenda vizuri ingawa pande zote mbili zimefanya siri.

Hata hivyo, hii inakumbushia sarakasi za mwaka 2023 baina ya timu hizo mbili kuhusu mambo kama haya.

Wakati wa sakata la Feisal Salum na Yanga tetesi zilikuwa zikisema Azam FC ndiyo wako nyuma ya kiburi cha mchezaji huyo na waajiri wake.

Katika kujaribu kuokoa jahazi, Yanga ilituma ujumbe kwa Azam FC kwa kuandika barua kutaka kuwanunua nyota wawili, Kipre Junior na James Akaminko.

Kisha barua hiyo ikavujishwa mitandaoni na kusambaa, halafu watu wenye ushawishi mitandaoni wakaja na ujumbe mmoja tu kana kwamba wamepewa mwongozo wa maneno (script).

Wote walisema maneno yanayofanana lakini wakiwasilisha ujumbe kama ni mawazo yao.

“Mimi ninavyoona Yanga haina haja na wachezaji hao, bali inataka kuifundisha Azam FC namna ya kufuata taratibu unapomhitaji mchezaji wa timu nyingine,” mojawapo wa ujumbe ulieleza hivyo.

Kuna uhuru wa mawazo, lakini watu wengi wakiwaza kwa kutumia maneno yanayofanana, kuna shaka.

Lengo hapa lilikuwa kuitia presha Azam FC iachane na Feisal Salum 'Fei Toto'. Sakata la Fei likaisha na kama yalivyosema mengi wakati ule akaangukia Chamazi.

Mwaka mmoja baadaye, picha imegeukia upande wa pili, Azam FC. Nyota wa Azam FC, Prince Dube amefanya yaleyale ya Fei. Hataki kuendelea kuitumikia klabu hiyo.


Na katika sakata hilo la Dube, Yanga ndiyo inatajwa kuwa nyuma ya kiburi cha mchezaji huyo kwa waajiri wake.

Azam FC nao wametuma barua Yanga kumtaka mchezaji huyo, lakini hapa hakuna ujumbe unaofuata wala shinikizo lolote bali wanataka kufanya biashara.

Barua ya Yanga ilikuwa inauliza kama Azam FC inaweza kuwauza wachezaji wale, lakini Azam FC haijatuma barua ya kuulizia bali ofa ya kumnunua yenye hadi kiasi cha bei ambayo wanataka kutoa.

Na kuonyesha kwamba wako siriazi, hawajavujisha barua mitandaoni wala hawajatumia watu wenye ushawishi kuweka shinikizo.

Taarifa za uhakika zinasema kocha wa Azam FC, Yousouph Dabo anamuona Mzize kuwa mshambuliaji anayetosha kwenye mfumo wake hivyo amewataka mabosi wake kuhakikisha anakuwa sehemu ya kikosi cha Chamazi msimu ujao.

Kazi aliyoionyesha Mzize kwenye mechi baina yao pale kwa Mkapa ilitosha kumshawishi Dabo kwamba ni mshambuliaji mzuri. Dabo amewasisitiza viongozi kwamba ana kazı na Mzize pale Azam Complex msimu ujao.