Azam waipa Simba winga

MATAJIRI wa Ligi Kuu Bara, Azam Fc walikuwa wakihusishwa kumtaka winga wa FC Platinum, Parfect Chikwende mara tu alipoonyesha kiwango bora katika mechi ya mzunguko wa kwanza Ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya Simba.

Ofisa mtendaji mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin 'Popat' alisema walikuwa na mpango wa kumsajili Chikwende ila baada ya benchi lao la ufundi lililokuwa chini ya kocha, George Lwandamina kutokuonyesha kumuhitaji wameamua kuachana na mpango huo.

"Tumeamua kuachana na mpango huo wa kumsajili Chikwende kutokana na Lwandamina kutaka straika na si winga nafasi ambayo anacheza mchezaji huyo kwa maana hiyo tumeachana mpango huo," alisema Popat.

Wakati Azam wakieleza kuachana na kutaka kumsajili Chikwende, taarifa zinaeleza winga huyo yupo hapa nchini tayari na amesha malizana na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara Simba.

Ripoti zinasema Simba wapo watayari kutoa  Dola 55, 000 ambazo ni zaidi ya sh 127 milioni  kwa ajili ya kupata huduma  mshambuliaji huyo wa zamani wa  Bulawayo Chiefs ,

Msemaji wa FC Platinum, Chido Chizondo akiwa  kwenye mahojiano na chombo kimoja cha habari nchini Zimbabwe alithibitisha kwa kusema Chikwende ameondoka Zimbabwe.

"Hatuwezi kuthibitisha kuwa ni klabu gani ameenda kujiunga nayo lakini tunaweza kusema kuwa ameondoka na kwenda Tanzania," alisema.

Chizondo aliongeza kwa kusema, "Simba wameweka mezani ofa lakini pia Azam nao wanaonekana kuvitiwa naye, tunasubiri kuona matokeo."

Simba  ilikuwa ilkiwafanyia majaribio katika michuano ya Mapinduzi,Wazimbabwe wawili ambao ni winga,  Ian Nyoni  na mchezaji wa zamani wa FC Platinum, beki Kelvin Moyo kwa ajili ya kuwajumuisha kwenye kikosi chao kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.