Azam wafungwa na URA 1-0, Kombe la Mapinduzi

Muktasari:
- Azam iliyopangwa kundi A pamoja na timu za Simba, Mwenge na Jamhuri za Pemba pamoja na URA ya Uganda waliyocheza nayo leo, itarudi uwanjani kesho Jumamosi kukipiga na Simba saa 02:15, usiku.
MABINGWA watetezi wa Kombe la Mapinduzi klabu ya Azam FC, imeshindwa kutamba kwenye mashindano hayo yanayoendelea kwenye Uwanja wa Amaan, Kisiwani Zanzibar baada ya kuchapwa bao 1-0 na URA ya Uganda.
URA ilipachika bao hilo dakika ya 32 kupitia kwa Kagaba Nicholas ambaye alipiga shuti kali lililompita tobo mlinda mlango wa Azam, Bedict Haule.
Hata hivyo, licha ya Azam kufanya mabadiliko ya kuwatoa, Yahya Zayd, Masoud na Paul Peter na nafasi zao kuchukuliwa na Salim Hoza, Mghana Enock Agyei na Shaaban Chilunda, waliambulia patupu.
Azam ilipata pigo dakika za lala salama baada ya mshambuliaji wao, Enock Agyei kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kurudishia rafu kwa makusudi.
Matajiri hao wa lambalamba wamepangwa kundi A, pamoja na timu za Simba, Mwenge na Jamhuri za Pemba pamoja na URA waliyocheza nayo leo, itarudi uwanjani kesho Jumamosi kukipiga na Simba saa 02:15, usiku.