Azam kuwachoma Wamisri

Muktasari:

AZAM na Simba zinakabiliwa na mechi za mtego leo na kesho katika mashindano ya klabu Afrika wakati zitakapocheza nyumbani na ugenini dhidi ya timu za Pyramids na Jwaneng Galaxy.

AZAM na Simba zinakabiliwa na mechi za mtego leo na kesho katika mashindano ya klabu Afrika wakati zitakapocheza nyumbani na ugenini dhidi ya timu za Pyramids na Jwaneng Galaxy.

Azam FC ambayo itakuwa nyumbani leo kwenye Uwanja wa Azam Complex kuanzia saa 9 alasiri kumenyana na Pyramids FC ya Misri. Waarabu hao watakuwa na kibarua kigumu cha kupangua ukali wa joto la mchana pamoja na mashambulizi mazito ya Azam ambayo imeonekana kujiamini zaidi.

Takwimu zinaonyesha katika mechi 10 zilizopita za mashindano ya kimataifa ambazo Pyramids FC ilicheza ugenini, imepata ushindi mara nane, sare moja na kupoteza mechi mbili tu huku ikifunga mabao 16 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano tu

Kocha msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati alisema hawatishwi na rekodi hiyo ya Pyramids na wamejipanga kuwatupa nje katika mashindano hayo.

‘Huu ni msimu mwingine na kila timu imejipanga. Tunawaheshimu Pyramids FC lakini hatuwaogopi. Tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunamaliza mechi hapa nyumbani na tunaamini uwezo huo upo. Hali ya kikosi ni nzuri na kila mchezaji yuko tayari,” alisema Bahati huku akisisitiza kwamba wamejipanga vizuri ndani na nje ya Uwanja. Alisema pia hata kitendo cha kuruhusiwa kuingiza mashabiki kwenye Uwanja wa Chamazi itasaidia kuwapa mzuka na wamepania kuimaliza mechi ndani ya ardhi ya nyumbani na muda uliopangwa ni muafaka kwao kwani wamejipanga.

Azam wanapaswa kuwa makini zaidi na mashambulizi kutokea pembeni mwa uwanja ambayo ndio yamekuwa yakitumiwa zaidi na Pyramids katika kutengeneza mabao yake.

Nyota za zamani wa Al Ahly na Brighton, Ramadan Sobhi ndiye mchezaji wa kuchunga zaidi katika kikosi cha Pyramids FC kutokana na uwezo wake binafsi wa kufunga mabao na kupiga pasi za mwisho.

Marefa kutoka Somalia ndio wamepangwa kuchezesha mchezo huo wa Azam dhidi ya Pyramids FC.

Wakati Azam wakirusha kete yao, Simba wao watakuwa ugenini huko Botswana kukabiliana na Jwaneng Galxy ya huko kesho.