Azam kusuka au kunyoa

Monday June 21 2021
namungo pic
By Ramadhan Elias

ACHANA na matokeo ya usiku wa jana wakati Yanga ikimalizana na Mwadui kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, jijini Dar es Salaam vumbi la Ligi Kuu Bara linaendelea leo kwa michezo miwili, huku Azam ikiwa na kibarua cha kusuka ama kunyoa juu ya hatma yao ya ubingwa msimu huu.

Azam itakuwa uwanjani mjini Lindi, kumenyana na wenyeji wao Namungo kwenye Uwanja wa Majaliwa, lakini mapema mchana KMC watakuwa wakijiuliza mbele ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo wa Dar unatrajiwa kuwa na ushindani wa aina yake, kwa vile wenyeji KMC ipo nafasi ya saba na inasaka tiketi ya kumaliza kwenye Nne Bora, kwa sasa ikiwa na pointi 41, nne zaidi na iliyonzo Mtibwa Sugar iliyoanza kujikongoja kuepuka kushuka daraja.

Lakini pambano la Ruangwa, Lindi ndilo bab’kubwa kutokana na wenyeji Namungo iliyopo nafasi ya sita ikiwa na pointi 42, itakapoikabili Azam inayoshika nafasi ya tatu na pointi zao 63 na inayohitaji ushindi ili kuendelea kuchelewesha mbio za ubingwa kwa vinara Simba na Yanga waliopo juu yao.

Mechi hii itapigwa saa 10:00 jioni huku kila timu ikihitaji ushindi huku Azam ikitamani alama tatu ili kuendelea kuishi kwenye mbio za ubingwa kwani itafikisha alama 66 na endapo itashinda mechi mbili zilizosalia itafikisha pointi 72 na kama Yanga na Simba zitapoteza mechi zao zote zilizosalia basi miujiza itawabeba kubeba ubingwa.

Kama itateleza kwa Namungo, maana yake Azam itaziachia Yanga na Simba ulingo wa kuchagua nan awe bingwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara.

Advertisement
Advertisement