Azam FC yatua kwa Mmorocco

Muktasari:

  • Taoussi aliyezaliwa Februari 6, 1959, inaelezwa yupo katika mazungumzo na viongozi wa timu hiyo na kama kila kitu kitaenda sawa basi atajiunga na matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam ili kukiongoza kikosi hicho kilichomaliza nafasi ya pili msimu uliopita na kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutolewa na APR.

MABOSI wa Azam FC wako katika harakati za kumsaka mrithi wa Yousouf Dabo aliyetimuliwa Septemba 3, mwaka huu kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo ndani ya kikosi hicho na sasa taarifa zinasema ipo katika mazungumzo ya kumnasa Kocha Rachid Taoussi, raia wa Morocco.

Taoussi aliyezaliwa Februari 6, 1959, inaelezwa yupo katika mazungumzo na viongozi wa timu hiyo na kama kila kitu kitaenda sawa basi atajiunga na matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam ili kukiongoza kikosi hicho kilichomaliza nafasi ya pili msimu uliopita na kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutolewa na APR.

Taarifa kutoka ndani ya Azam, zimelidokeza Mwanaspoti kwamba, Taoussi ni miongoni mwa makocha wanaoweza kujiunga na kikosi hicho ikiwa makubaliano baina ya pande zote mbili yatafikiwa, ingawa wapo wengine ambao pia wameomba nafasi hiyo.

“Kila kitu kinaenda vizuri hadi sasa katika mchakato wa kumpata kocha mpya ingawa hatutaki kufanya maamuzi ya haraka kwa sababu tunahitaji kupata mtu sahihi atakayeleta mabadiliko ya kiuchezaji kikosini,” kilisema chanzo kutoka ndani ya timu hiyo.

Kwa upande wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Abdulkarim Amin ‘Popat’, alisema, taarifa yao ya mwisho inaeleza kila kitu na sasa kikosi hicho kitaendelea kufundishwa na makocha wa timu za vijana chini ya Kassim Liogope na Mohamed Rijkaard.

Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua kwamba mabosi wa kikosi hicho walianza mazungumzo na Juma Mgunda anayeifundisha Simba Queens na Florent Ibenge wa Al Hilal ya Sudan ingawa dili hilo linaweza kukwama kutokana na mahitaji ya Mkongomani huyo.

Taoussi ambaye enzi za uchezaji wake alikuwa kiungo, ameifundisha timu ya taifa ya Morocco chini ya miaka 17, 20 na 23, huku akiwa kocha msaidizi ndani ya kikosi hicho pamoja na kuhudumu kama Mkurugenzi wa Ufundi.

Mbali na kuhudumu katika timu ya taifa, Taoussi amewahi pia kuzifundisha klabu kadhaa zikiwemo RS Berkane, FAR Rabat, Raja Casablanca, Olympique Club de Khouribga na Wydad Casablanca zote za Morocco na ES Setif kutoka Algeria. Akiwa na Maghreb de Fes cha Morocco aliipa ubingwa wa Trone mwaka 2011.