Azam FC yaendelea kusainisha majembe

Muktasari:
- Jioni hii klabu hiyo imeachia picha za usajili wa kiungo mshambuliaji mpya Djibril Sillah 'The Killer' kutoka klabu ya Raja Canablanca ya Morocco.
KLABU ya Azam FC imeendelea kusainisha majembe mapya kwa msimu ujao wa Ligi Kuu na michuano mingine ikiwamo ya kimataifa, sambamba na kuwaongezea mikataba nyota waliokuwepo kwenye kikosi kilichomaliza nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na Simba katika ligi ya msimu uliopita.
Jioni hii klabu hiyo imeachia picha za usajili wa kiungo mshambuliaji mpya Djibril Sillah 'The Killer' kutoka klabu ya Raja Canablanca ya Morocco.
Huyo ni mchezaji wa pili kukamilisha dili la kujiunga na Azam baada ya Feisal Salum 'Fei Toto' aliyenyakuliwa kutoka Yanga hivi karibuni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na klabu hiyo iliyopanda Ligi Kuu msimu wa 2008-2009, ilisema kuwa, Sillah amekamilisha taratibu za kujiunga na klabu yetu baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili akitokea @RCAofficiel.
Nyota huyo raia wa Gambia ametua klabu hapo wakati nyota wa kikosi hicho kwa msimu uliopita wakiongezewa mikataba mipya baada ya ile waliyokuwa nayo kumalizika akiwamo James Akaminko, Malickou Ndoye, Nathaniel Chilambo, Daniel Amoah, Idris Mbombo, Sospeter Bajana, Abdallah Kheri 'Sebo' na Lusajo Mwaikenda.
Wakati wachezaji hao wa zamani wakiongezwa mikataba na wapya wakianza kutambulishwa, nyota wengine saba waliokuwa na timu hiyo wameshapewa 'Thank You' mapema sambamba na makocha waliokuwa wakiinoa Azam FC ili kupisha kusukwa kwa kikosi kipya chini ya Kocha Youssof Dabo.
Waliotemwa ni pamoja na Rodgers Kola, Aggrey Morris, Ismail Aziz Kader, Kenneth Muguna, Bruce Kangwa, Cleophas Mkandala na kipa Wilbol Maseke.