Azam FC, Mashujaa hakuna mbabe Chamazi

Muktasari:

  • Azam iliingia katika mchezo huu ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Namungo huku kwa upande wa Mashujaa ikitoka kuchapwa 2-1 mbele ya Coastal Union.

MCHEZO wa Ligi Kuu Bara kati ya Azam FC na Mashujaa umemalizika kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi Kwa timu hizo kutoka suluhu.

Azam iliingia katika mchezo huu ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Namungo huku kwa upande wa Mashujaa ikitoka kuchapwa 2-1 mbele ya Coastal Union.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza baina ya timu hizo uliopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma, Azam ilishinda mabao 3-0.

Mabao ya Azam katika mchezo huo uliopigwa Novemba Mosi mwaka jana, yalifungwa na Kipre Junior, Gibril Sillah na Alassane Diao ikiwa ni mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara kwa timu hizo kukutana.

Kwa matokeo haya yanaifanya Azam kufikisha jumla ya michezo 23 ambapo kati ya hiyo imeshinda 15, sare sita na kupoteza miwili ikiendelea kusalia nafasi ya pili na pointi 51.

Pointi hizo ni pungufu ya nne na vinara wa Ligi Kuu Bara na mabingwa watetezi Yanga yenye 55 huku ikiwa pia na faida ya michezo miwili kwani hadi sasa imecheza jumla ya mechi 21.

Kwa upande wa Mashujaa katika michezo yao 23 iliyocheza, imeshinda mitano tu, sare saba na kupoteza 11 ikiendelea kusalia nafasi ya 15 na pointi 22.

Matokeo mengine ya michezo ya leo, Geita Gold ililazimishwa suluhu na Maafande wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Nyankumbu Geita huku Tabora United ikichapwa mabao 3-0 na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora.

Mabao ya Kagera Sugar katika mchezo huo yalifungwa na Moubarack Amza dakika ya 24, Obrey Chirwa dakika ya 48 na Mbaraka Yusuph dakika ya 72.

Kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi, wenyeji Namungo iliyochapwa na Azam FC mabao 2-0, mechi iliyopita ilizinduka leo na kuifunga Coastal Union bao 1-0, lililofungwa na nyota wa timu hiyo, Hassan Kabunda dakika ya nane.