Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Azam FC inavyojipanga kutetea taji la Kagame

BINGWA mtetezi wa Kombe la Kagame, Azam FC leo Ijumaa ataanza kutetea kombe lake kwa kuivaa Kator ya Sudan ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex, uwanja ambao imeuzoea kucheza.

Azam ilifanikiwa kutwaa ubingwa huo mwaka 2015 ambapo baada ya hapo mashindano hayo hayakufanyika kutokana na sababu mbalimbali za waandaji, hivyo Azam msimu huu wana kazi ya kuwaonyesha Watanzania juu ya uwezo wao wa kutetea taji hilo.

Kuna mabadiliko mengi yamefanyika ndani ya kikosi cha Azam FC tangu watwae ubingwa huo kwani baadhi ya wachezaji wao nyota ambao walifanikiwa kutwaa ubingwa huo hawapo ndani ya kikosi na kwa asilimia kubwa wamehamia Simba ambao ni John Bocco, Aishi Manula, Shomary Kapombe na Erasto Nyoni.

Mwaka 2015 walitwaa kombe hilo bila kupoteza mchezo wowote katika mechi zote sita, kwa kuanza kuifunga KCCA 1-0, Al-Malakia 2-0 na Adama City 5-0 kwenye hatua ya makundi na kufuzu robo fainali.

Bocco na Kipre Tchetche ndiyo walifanikisha ubingwa huo kwa kufunga mabao 2-0 Gor Mahia. Azam ilitwaa kombe hilo ikiwa na historia ya kutwaa ubingwa bila kuruhusu bao kwenye mashindano hayo.

Kwa sasa Azam FC inahangaika jinsi ya kutetea ubingwa huo kutokana na kikosi kilichopo chenye mabadiliko makubwa ambapo Mwanaspoti linakuletea baadhi ya mambo ambayo yanapaswa kufanywa na Azam FC ili kutetea ubingwa wao.

KIKOSI KUPANGUKA

Kikosi takriban chote ambacho kimecheza mashindano ya mwaka 2015, leo hii hakipo kwani hata wachezaji waliofunga mabao katika fainali nao hawapo. Hivyo kuna kazi kubwa ya wachezaji waliopo kudhihilisha ubora wao wa kusajiliwa ndani ya matajiri hao wa ligi nchini.

Tangu wachezaji hao waondoke ndani ya Azam, kikosi hicho kimekuwa kikienda kwa kusuasua ingawa hivi sasa wameonekana kufanya usajili ambao unaweza kuwabeba kwenye msimu ujao na hata mashindano haya ya Kagame kama watawatumia.

WACHEZAJI WAPYA HAWAJAFITI

Baada ya msimu kumalizika ilimchukua Kocha Hans Pluijm kutoka Singida United lakini hata hivyo, kocha huyo hatakuwepo katika benchi la ufundi litakalosimama kwenye mashindano hayo.

Mpaka sasa Azam FC imewasajili nyota wapya, Nicco Wadada, Tafadzwa Kutinyu, Donald Ngoma, Ditram Nchimbi, Mudathir Yahya ambao wana uhakika wa kucheza mashindano hayo huku Ngoma na Kutinyu hawatakuwa katika kikosi hicho kwa sababu tofauti.

Nchimbi na Wadada ni wapya tofauti na Mudathir ambaye ndio nyumbani kwake, hivyo kivyovyote kutakuwa na changamoto ya ugeni kwani bado hawajazoeana vizuri na wenzake kwenye mfumo wa uchezaji sambamba na Wadada ambaye ni mzoefu ila alichelewa kujiunga na wenzake kwenye maandalizi yao.

BENCHI JIPYA LA UFUNDI

Msimu uliopita Azam ilikuwa na Kocha Aristica Cioba, lakini hakukaa sana na kuondoka kurejea kwao Romania na kumuachia timu msaidizi wake Idd Cheche.

Cheche alipambana na kufanikiwa kumaliza nafasi ya pili licha ya kusuasua.

Hivi sasa benchi la Ufundi limebadilika licha ya kwamba Pluijm hatakuwepo katika mashindano haya ila Cheche atakuwa na kibarua kizito mbele ya Juma Mwambusi, wote ni makocha wasaidizi.

Bado haijafahamika mara moja mfumo utakaotumika kwani Cheche amekuwa akitumia mfumo wa kuweka mpira chini na kupiga pasi nyingi, lakini Pluijm ambaye aliwahi kufanya kazi na Mwambusi huwa anapenda mpira wa kushambulia sana tena kwa kasi.

UBUTU WA WASHAMBULIAJI

Licha ya kwamba kumaliza nafasi ya pili katika ligi, ukweli ni kwamba katika safu yake ya ushambuliaji haikuwa nzuri sana.

Vijana Shaaban Idd na Yahya Zaid hawakuwa makini sana katika kufunga na hilo lipo wazi, kwani mabao yao yalikuwa yakifungwa na Idd Kipagwile, Frank Domayo na wachezaji wengine ambao hawakuwa washambuliaji katika kikosi hicho.

Katika washambuliaji ambao wamewasajili na watacheza mashindano haya ni Ditram Nchimbi pekee, uwezo wake wa kupambana na kulijua goli kunaweza kukaisaidia lakini kama Shaban Chilunda na Zaidy watashindwa kuonyesha itakuwa shida nyingine.

Kurejea kwa Wazir Junior ambaye alikuwa majeruhi msimu uliopita, huu ndio muda wake wa kuonyesha kama akipata nafasi ya kucheza kwani bado anadaiwa na kikosi hicho kutokana na kushindwa kuifanyia kazi timu yake vizuri pamoja na Mbaraka Yusuph aliyesajiliwa kuziba pengo la Bocco ila bado hajaonyesha makali yoyote, hivyo kupitia michuano hiyo ana kibarua cha kufanya.

KOCHA AFUNGUKA

Kocha msaidizi wa kikosi hicho Idd Cheche, alisema kwamba kutokana na ufupi wa ratiba ya maandalizi, imewalazimu kufanya mazoezi ya nguvu ili kufanya vizuri katika mashindano hayo.

“Tumekuwa na namna tofauti za kufanya mazoezi ili kuhaiikisha tunakuwa vizuri katika mashindano haya, uchache wa kujiandaa ulikuwa karibu sana lakini tupo vizuri, naamini tutatetea ubingwa wetu,” alisema.