Ayoub aiwahi Yanga

Muktasari:

  • Kwenye mechi mbili alizokosekana Ayoub nafasi yake ilichukuliwa na Ally Salim ambaye ameshindwa kuibeba Simba ikiondolewa hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho (FA) na Mashujaa kwa penalti 5-4 na kuambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Ihefu FC katika mechi ya Ligi Kuu Bara.

BAADA ya kukosekana kwenye mechi mbili ya ligi na Kombe la Shirikisho 'FA', timu yake ikidondosha pointi, kipa namba moja wa Simba Ayoub Lakred amejiunga na wenzake kwa ajili ya kambi mjini Zanzibar kujiandaa na mchezo dhidi ya Yanga utakaopigwa Jumamosi wiki hii.

Kwenye mechi mbili alizokosekana Ayoub nafasi yake ilichukuliwa na Ally Salim ambaye ameshindwa kuibeba Simba ikiondolewa hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho (FA) na Mashujaa kwa penalti 5-4 na kuambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Ihefu FC katika mechi ya Ligi Kuu Bara.

Ayoub ambaye mechi yake ya mwisho kucheza ilikuwa dhidi ya Al Ahly ugenini wakiondolewa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa mabao 2-0 ugenini na nyumbani bao 1-0, alirudi nchini Jumamosi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Simba  Abbas Suleiman amesema kipa huyo ambaye alirudi nchini kwao kwa matatizo ya kifamilia amerudi na leo Mwanaspoti limemshuhudia akiwa miongoni mwa wachezaji waliosafiri na kikosi hicho kwenda Zanzibar.

"Ayoub tayari amesharudi na amejumuika na wenzake tayari kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa Jumamosi dhidi ya watani Yanga na mechi nyingine za ligi zilizobaki, suala la kucheza au kutocheza lipo chini ya kocha," amesema.

Kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola amesema timu imeanza mazoezi tayari kwa ajili ya mchezo dhidi ya Yanga aliodai kuwa ni muhimu kwao kurudisha molari ya ushindi baada ya kukosa matokeo kwenye mechi nne mfululizo.

"Timu ilipata mapumziko siku moja baada ya kutoka Singida, sasa tunaendelea na maandalizi ya mchezo kuelekea mechi ya Jumamosi ambao sio rahisi kwetu tunahitaji kujiandaa vizuri ili kuhakikisha tunaonyesha mchezo bora na wa ushindani," amesema.

"Matatizo yaliyoonekana kwenye mechi nne zilizopita yanaendelea kufanyiwa kazi na benchi la ufundi huku akikiri kuwa washambuliaji ndio wanaowaangusha kutokana na kushindwa kutumia nafasi wanazotengeneza."

Matola amesema licha ya kupoteza mechi hizo, lakini timu imekuwa ikitengeneza nafasi, lakini inashindwa kuzitumia hilo wao kama benchi la ufundi wameliona na tayari wameanza kulifanyia kazi kabla ya kuwakabili watani zao.