Aucho atemwa, Mukwala aitwa The Cranes

Muktasari:
- Michezo hiyo ambayo inaonekana ni maalum kwa ajili ya kujiandaa na mashindano mbalimbali mojawapo ni Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza katika Ligi za Ndani (CHAN) itafanyika Juni 6 na Juni 9 mtawalia.
Kiungo wa Yanga, Khalid Aucho hayupo katika orodha ya wachezaji 28 walioitwa na timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ kwa ajili ya mechi mbili za kimataifa za kirafiki dhidi ya Cameroon na Gambia zitakazochezwa mwezi ujao huko Morocco.
Michezo hiyo ambayo inaonekana ni maalum kwa ajili ya kujiandaa na mashindano mbalimbali mojawapo ni Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza katika Ligi za Ndani (CHAN) itafanyika Juni 6 na Juni 9 mtawalia.
Juni 6, Uganda itacheza na Cameroon na Juni 9 itakabiliana na Gambia mechi zote zikichezwa jijini Marrakech, Morocco na Aucho ambaye ni nahodha wa Uganda hatokuwepo kwa vile kocha mkuu Paul Put hajamjumuisha kikosini.
Kiungo huyo wa Yanga alikuwa nje ya uwanja kwa takribani mwezi mmoja kutokana na majeraha ya nyama za paja.
Mshambuliaji wa Simba, Steven Mukwala ni miongoni mwa nyota 28 walioitwa katika kikosi hicho ambacho kina wachezaji 12 tu wanaocheza katika Ligi ya Uganda.