Prime
Aucho akoleza mzuka Yanga

Muktasari:
- Kiungo huyo tegemeo raia wa Uganda, aliumia Aprili 7 katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union ambapo watetezi hao, waliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Pacome Zouzoua na kumfanya akose mechi mbili zilizofuata za ligi dhidi ya Azam FC na Fountain Gate.
KIKOSI cha Yanga kimesharejea jijini Dar es Salaam kikitokea Pemba, Zanzibar kilipoenda kushiriki michuano ya Kombe la Muungano na kuibuka mabingwa kwa kuifunga JKU kwa bao 1-0, huku kiungo wa timu hiyo, Khalid Aucho akikoleza mzuka.
Kiungo huyo tegemeo raia wa Uganda, aliumia Aprili 7 katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union ambapo watetezi hao, waliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Pacome Zouzoua na kumfanya akose mechi mbili zilizofuata za ligi dhidi ya Azam FC na Fountain Gate.
Hata hivyo, taarifa njema kwa mashabiki wa Yanga ni kwamba Aucho aliyekuwa anasumbuliwa na jeraha la nyama la pja, ameanza mazoezi ikiwa ni ishara ya kuiwahi mapema mechi nne zilizosalia za kumaliza msimu ikiwamo Dabi na huenda kaanza kwanza na Namungo iliyopangwa kupigwa Mei 13.
Akizungumza na Mwanaspoti, Aucho amethibitisha tayari amepona na amerudi katika hali ya utimamu akianza mazoezi mepesi na anaushukuru uongozi na madaktari kwa kufanya kazi yao na kumsaidia kurwejea kwenye majukumu yake ya kawaida.
“Haikuwa nzuri kwangu kuwa nje ya uwanja kwa muda kutokana na majeraha, lakini nashukuru kwa sasa nimerejea uwanjani. Hii ni njema kwangu na kwa Yanga pia kwani naamini kuna umuhimu wa mimi kutumikia mkataba wangu,” alisema Aucho na kuongeza;
“Kuanza mazoezi ni hatua nzuri suala la kucheza naliachia benchi la ufundi lakini nafurahi nimerudi na nipo tayari kuipambania timu yangu iweze kufikia malengo ya kutetea taji tunalolishikiria.”
Mbali na mechi mbili alizokosa kuitumikia Yanga katika Ligi Kuu ikiwamo ile ya Azam waliowanyoa kwa mabao 2-1 kisha kuifunga Fountain Gate kwa mabao 4-0, pia Aucho hakuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kikilichoshiriki Kombe la Muungano na kubeba taji usiku wa juzi.
Aucho alikosa pia mechi za robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Stand United ambapo Yanga ilishinda mabao 8-1 na kukata tiketi ya nusu fainali ambapo sasa itaivaa JKT Tanzania siku ya Mei 16 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
Kurejea kwa Aucho mbali na kuiwahi Namungo, lakini itamfanya aziwahi mechi nyingine tatu za Ligi Kuu ikiwamo Dabi ya Kariakoo ambayo bado haifahamiki itapigwa wapi, sambamba na mechi ya nusu fainali ya Shirikisho (FA), timu hiyo ikiwa watetezi wa taji inalolishikilia kwa misimu mitatu mfululizo.
Mechi ya Dabi ilishindwa kufanyika Machi 8 baada ya kuahirishwa na Bodi ya Ligi saa chache kabla ya kufanyika kwake kutokana na kilichoelezwa kuzuiwa kwa Simba kufanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa mbali na maelezo ya kuwepo kwa viashirai vya rushwa.
Kuhusu mkataba alionao na Yanga unaelekea mwishoni, Aucho alisema kwa sasa yeye ni mchezaji wa Yanga, hivyo hawezi kusema lolote kwa sasa zaidi ya kuipambani timu itetee mataji.
Aucho alisajiliwa na Yanga mwaka 2021 akitokea Masr El Makasa ya Misri na amekuwa mhimili mkuu wa timu hiyo akiiwezesha kubeba mataji matatu ya Ligi Kuu Bara, matatu ya Kombe la Shirikisho na kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2022-2023 iliyopoteza kwa kanuni ya bao la ugenini mbele ya USM Alger ya Algeria baada ya kutoka sare ya 2-2 kwa matokeo ya mwisho.