Aucho afurahia kutangaza ubingwa mbele ya Simba

Muktasari:
- Aucho ambaye msimu wa 2023/24 alicheza mechi 20 kwa dakika 1629 na kutoa asisti mbili, na 2024/25 amefunga bao moja dhidi ya Mashujaa Yanga iliposhinda mabao 5-0, amesema kuifunga Simba na kunyakua taji ni kitu cha kipekee na chenye mvuto wa aina yake.
KIUNGO wa Yanga, Khalid Aucho amesema kitu kilichomfurahisha zaidi kwa msimu ulioisha ni kitendo cha kunyakua taji la ubingwa wa Ligi Kuu Bara mbele ya Simba, jambo lililodhihirisha ubora wao.
Aucho ambaye msimu wa 2023/24 alicheza mechi 20 kwa dakika 1629 na kutoa asisti mbili, na 2024/25 amefunga bao moja dhidi ya Mashujaa Yanga iliposhinda mabao 5-0, amesema kuifunga Simba na kunyakua taji ni kitu cha kipekee na chenye mvuto wa aina yake.

"Simba ni klabu kubwa yenye ushindani wa Ligi ya ndani hadi michuano ya kimataifa pia bato kali baina yake na Yanga,hivyo kuifunga na kutangaza ubingwa mbele yake kinaleta raha ya aina yake," amesema Aucho na kuongeza:
"Hakuna kitu kizuri unapofanikiwa mbele ya mshindani wako, inapandisha wasifu wa wachezaji na huenda tukio hilo lisijitokeze miaka ya hivi karibuni, kutangazwa mabingwa mechi ambayo umekutana na mtani wako wa enzi na enzi."
Aucho amesema msimu ulioisha ni wa kihistoria kwa Yanga kuifunga Simba ndani na nje, na pia kunyakua mataji yote ya mashindano makubwa nchini.
Misimu minne aliyocheza Aucho Yanga tangu alipojiunga nayo msimu 2021-2025 amefanikiwa kunyakua mataji manne ya Ligi Kuu Bara pamoja na ya Kombe la FA.

"Nimekuwa na wakati mzuri tangu nilipojiunga Yanga, imekuwa na mafanikio ya kuchukua mataji, kama mchezaji inaniongezea CV kubwa katika kazi ninayoifanya," amesema Aucho ambaye kuna taarifa za ndani zinaeleza ameanza kufanya mazungumzo ya kuongezewa mkataba mpya na viongozi wa Yanga.