Aubameyang akiondoka kwenda Barcelona, hawa wanakuja Arsenal kupiga mzigo

Muktasari:
Kuna orodha ndefu ya mastaa wanaofaa kabisa kwenda kuvaa buti za Aubameyang kama ataondoka Emirates, wakiongozwa na straika mkongwe, Edinson Cavani.
LONDON, ENGLAND. BARCELONA imetangaza wazi kwamba inahitaji straika mpya ndani ya dirisha hili la uhamisho wa Januari.
Straika wao namba moja, Luis Suarez ameumia na wenyewe wanataka mtu wa kuja kuchukua mikoba yake iwe kwa kumbeba jumla au kwa kumsajili kwa mkopo, kinachotakiwa fowadi mpya atue Nou Camp.
Huko na huko, macho yameangukia kwa straika wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang. Rais wa Barca, Josep Maria Bartomeu, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu, Oscar Grau, Mkurugenzi wa soka, Eric Abidal, Mkurugenzi wa ufundi, Ramon Planes na kocha Quique Setien wote wamekubaliana kwamba Aubameyang anafaa kwenda kuziba pengo la majeruhi Suarez.
Hilo likitokea itakuwaje huko Emirates? Kocha Mikel Arteta kwa sasa tu anahaha baada ya fowadi wake huyo kutumikia adhabu ya mechi tatu baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu, sasa itakuwaje kama Barca watakuja kumbeba jumla? Straika wake mwingine kwenye kikosi, Alexandre Lacazette amekuwa hana makali, akiwa amefunga mabao matano tu na asisti mbili msimu huu.
Hakuna namna, Arteta hatakuwa na ujanja zaidi ya kuingia sokoni kunasa fowadi mpya kama Aubameyang atang'oka kwenda kucheza timu moja na Lionel Messi huko Nou Camp. Kuna orodha ndefu ya mastaa wanaofaa kabisa kwenda kuvaa buti za Aubameyang kama ataondoka Emirates, wakiongozwa na straika mkongwe, Edinson Cavani.
Ripoti zinadai kwamba Cavani yupo tayari kuachana na PSG akiandika barua ya kuomba kuondoka, hivyo Arsenal wanaweza kwenda kunasa saini yake kwa haraka kuja kuziba pengo la Aubameyang kama ataamua kutimka. Mastaa wengine ambao Arteta anaweza kuwageukia ni pamoja na Wilfried Zaha, Thomas Lemar, Moussa Dembele, Krzysztof Piatek na Timo Werner.
Ugumu utakuwa kwa Zaha katika kuwashawishi Crystal Palace, lakini kwa Lemar na Piatek hakutakuwa na tatizo baada ya timu zao, Atletico Madrid na AC Milan kuwa tayari kuwaruhusu mastaa hao watakapotaka kuondoka.
Dembele huko Lyon wanadaiwa kuweka ngumu staa wao kuondoka ndani ya dirisha hili la majira ya baridi huko Ulaya, lakini kwa RB Leipzig hawatakuwa na tatizo kama Werner mwenyewe atakuwa tayari kwenda kukipiga Arsenal na mabosi wa Emirates wakiwa tayari kuweka mezani mkwanja wanaoutaka. Mastaa hao ndio wanaotajwa kwamba huenda wakaenda kufiti kwenye kikosi cha Arsenal endapo Aubameyang ataamua kwenda kujaribu bahati yake huko Nou Camp kama mabosi wa huko watakwenda kubisha hodi Arsenal kutaka huduma yake.