Aston Villa wamtibulia Klopp

Muktasari:

Liverpool ndio mabingwa wa kwanza wa Ligi Kuu England maarufu kama EPL kufungwa mabao saba tangu Septemba 1953.

LONDON, ENGLAND. KITENDO cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Liverpool kutandikwa mabao 7-2 dhidi ya Aston Villa kimemtibua kocha wa timu hiyo, Jurgen Klopp na kusema ni aina mbaya ya historia ambayo wameitengeneza.

Katika mchezo huo ambao ulichezwa Villa Park aliyekuwa mwiba kwa Liverpool alikuwa Ollie Watkins aliyefunga mabao matatu na Jack Grealish aliyetupia mawili.

Klopp amesema kwa msimu uliopita hawajapoteza mchezo wowote hadi pale ambapo Watford walipolipiza kisasi lakini msimu huu imekuwa tofauti.

Ndani ya mechi nne tu, wamekumbana na kipigo cha kihistoria, "Nani alitaka tupoteze kwa mabao 7-2? Mwaka jana tulikubaliana kuweka historia lakini naona imekuwa historia mbaya.

"Kuna nafasi ambazo hatukuzitumia lakini haitoshi kusema kuwa tulikuwa na uwezo wa kutoka hata sare ya mabao 7-7, tumefanya makosa mengi ambayo yametugharimu," amesema kocha huyo.

Klopp ameendeleea kuongelea kipigo hicho kwa kusema, "Tulipoteza mipira katika eneo lisilofaa na hatukulinda vizuri. Kwa kawaida unaweza kuwa 1-0 nyuma na kufanya unachotaka ili kukomboa

"Tulijitahidi kucheza lakini hatukujilinda ipasavyo kwa hivyo kila mpira tuliopoteza ulikuwa shambulio kubwa kwetu. Hakuna mtu wa kulaumu isipokuwa mimi na wachezaji wote kwa kilichotokea," amesema.

Mlindalango chaguo la kwanza la Liverpool, Alisson alikosekana kwenye mchezo huo kutokana na kuuguza jeraha la bega na mbadala wake Adrian ndiye aliyecheza mchezo huo ambao wamekumbana na kipigo cha mbwa koko (7-2).

Klopp ameeleza kwamba mlinda mlango huyo wa Brazil ana uwezekano wa kurudi katika hali ya usawa mara tu baada ya mapumziko ya wiki ya kimataifa.