ASFC kuna mechi za visasi

MBEYA. BINGWA mtetezi wa Azam Sports Federation (ASFC) Yanga itakuwa mwenyeji wa Geita Gold katika mchezo wa robo fainali utakaopigwa Aprili huku timu hizo zikiwa na visasi vya aina yake.

Msimu uliopita wakati Yanga ikinyakua ubingwa iliisambaratisha Geita Gold Uwanja wa Mkapa katika hatua hii ya robo fainali baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1 Yanga ikinufaika kwa penalti 7-6.

Hata hivyo kabla timu hizo hajakutana Aprili kwenye ASFC zimetoka kukutana kwenye mchezo wa Ligi Kuu wiki iliyopita Uwanja wa Azam Complex na Yanga kushinda kwa mabao 3-1.
Ukiacha mchezo uliopita Yanga katika michezo mitatu ya nyuma ilikuwa inashinda bao 1-0 hivyo mchezo ujao wa ASFC unaonekana kuwa na ushindani zaidi zitakapokutana.

Mchezo mwingine utakaokua na mvuto wa aina yake ni ule wa Simba dhidi ya Ihefu ambayo baada ya kukutana kwenye ASFC zitakutana tena siku chache Uwanja wa Highland Estates, Mbarali kwenye mchezo wa Ligi Kuu.

Katika michezo mitatu ya Ligi Kuu walizokutana, Ihefu imepoteza michezo yote na katika michezo hiyo imeambulia bao moja pekee kwenye kichapo cha mabao 2-1 Septemba 6, 2020 bao lililofungwa na Omary Mponda, huku yale ya Simba yakifungwa na Mzamiru Yasin pamoja na John Bocco.

Kocha wa Ihefu, Zuberi Katwila alisema huo utakuwa mchezo wa aina yake sababu ni mchezo ambao unaleta hisia tofauti kwa kila timu kutokana na ubora wa vikosi walivyo navyo.
Mbeya City inayokutana na Singida Big Stars, kutinga robo fainali ndio mafanikio yake makubwa kwenye ASFC tangu ilipopanda Ligi Kuu msimu wa mwaka 2013/14 chini ya kocha Juma Mwambusi.

Msimu uliopita Mbeya City ilitolewa hatua ya kwanza na African Lyon kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya mabao 2-2 na mara ya mwisho kukutana na Singida Uwanja wa Liti ilikuwa Agosti 20 mwaka Jana na Mbeya City kuchapwa bao 1-0.
Kocha msaidizi wa Mbeya City, Anthon Mwamlima alisema hadi kufika hatua hiyo ni mafanikip makubwa kwao sababu misimu yote walikuwa wakiishia hatua za awali lakini sasa wapo robo fainali.

Mshindi kati ya Simba na Ihefu itacheza na mshindi kati ya Azam na Mtibwa katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali utakaochezwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
Endapo Simba na Azam zikakutana katika nusu fainali utakuwa mchezo wa kisasi baada ya Simba kuichapa Azam bao 1-0 katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa Uwanja wa Majimaji, Songea Juni 21, 2021.

Kama Simba na Yanga zikifanikiwa kutinga fainali utakuwa mchezo wa kisasi kwa mara nyingine kwani mara ya mwisho kwenye fainali kukutana Simba iliichapa Yanga bao 1-0 Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma Julai 25, 2021.

Azam na Yanga nazo zikifanikiwa kupenya hadi fainali utakua mchezo wa vita kwani mara ya mwisho zilikutana fainali msimu wa mwaka 2015/16 na Yanga kushinda mabao 3-1.

Lakini Mtibwa na Singida Big Stars zikifanikiwa kupenya fainali nazo zitakuwa zikirejesha kumbukumbu ya msimu wa mwaka 2017/18 katika fainali iliyopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha na Mtibwa kutwaa ubingwa japo msimu huo ilikuwa ikiitwa Singida United.

Mabingwa wa ASFC
2015/16 - Yanga 3-1 Azam
2016/17 - Simba 2-1 Mbao FC
2017/18 - Singida 2-3 Mtibwa Sugar
2018/19 - Lipuli FC 0-1 Azam FC
2019/20 - Simba 2-1 Namungo
2020/21 - Yanga 0-1 Simba
2021/22 - Yanga 3-3 Coastal Union (4-1 penalti).