ASEC haitoboi kwa Simba 

Muktasari:

  • Simba inahitaji ushindi kwenye mchezo huo ili kuweka hai hesabu za kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikijua wazi ASEC inataka heshima tu kumaliza kinara wa Kundi B ikiwa imeshafuzu baada ya kufikisha pointi 10.

Simba imetua Ivory Coast tayari kwa maandalizi yao ya mwisho kabla ya kukutana na wenyeji wao ASEC Mimosas, lakini kuna mambo mawili mapema tu yameanza kuwabeba wekundu hao.


Simba inahitaji ushindi kwenye mchezo huo ili kuweka hai hesabu za kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikijua wazi ASEC inataka heshima tu kumaliza kinara wa Kundi B ikiwa imeshafuzu baada ya kufikisha pointi 10.


Hata hivyo, mapema tu hesabu zimeanza kuibeba Simba nje ya uwanja baada ya wekundu hao kuwa tayari kimchezo na imecheza mechi tano za ligi kuanzia Februari 3, 2024, iliposhinda ugenini dhidi ya Mashujaa.

Simba hatari ugenini:
Simba imeshinda mechi  zote nne ugenini na kuvuna jumla ya pointi 12, kisha ikalazimishwa sare nyumbani dhidi ya Azam FC na kufanya timu hiyo kukusanya alama 13 ndani ya mechi tano.


Iko hivi, mechi hizo zitakuwa zimewajenga Simba kwa ajili ya mechi yao na ASEC ambao tangu mwaka huu uanze haijacheza mechi yoyote ya mashindano ingawa imekuwa ikicheza mechi kadhaa za kirafiki.


Mara ya mwisho ASEC kucheza mechi ya mashindano ni Desemba 30 ikishinda nyumbani bao 1-0 dhidi ya Stade d’Abidjan la mkwaju wa penalti iliyopigwa na kiungo Serge Pokou na ndiye staa wa kuchungwa na Simba.


Simba bora:
ASEC ikiangalia hata msimamo wa ligi ya hapa itashtuka kwani Simba ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 36, baada ya kucheza mechi 16, ambazo ni alama 10 zaidi ya zile ambazo inazo wapinzani wao waliopo nafasi ya nne na pointi 26 baada ya kucheza mechi 15.


Simba pia ina safu ya ushambuliaji inayofunga mabao kwani kwenye ligi imeshafunga mabao 31 huku ikiruhusu 14, wakati wenyeji wao hao mpaka ligi yao inasimama kupisha Fainali za Mataifa Afrika Afcon 2023, zilizofanyika nchini kwao ilikuwa imefunga mabao 20 na kuruhusu 10.


Pigo kubwa kwao:
Pigo kubwa kwa ASEC ni mshambuliaji wao kinara wa mabao Sankara Karamoko ambaye alishafunga mabao sita kwenye Ligi ya Mabingwa hatakuwa sehemu ya mchezo huo kwa mara ya kwanza, baada ya kuuzwa kwenda klabu ya Wolfsberger AC ya Austria kwenye usajili wa dirisha dogo, ndiye aliyetoa asisti wakati Simba ikilazimishwa sare nyumbani na miamba hiyo kutoka Afrika Magharibi.

Freddy anawajua haswa:
Mshambuliaji wa Simba Freddy Koublan amewatuliza mashabiki kuhusu mchezo huo, akiwaambia anawafahamu vilivyo wapinzani wao hao.


Akizungumza na Mwanaspoti alisema safari ya kwenda Ivory Coast kwa ajili ya mechi hiyo kwake ni furaha kwani anaona kama ameanza vizuri michuano hiyo kutokana na kuwafahamu wapinzani wao.


Freddy ambaye hajawahi kuchezea ligi ya Ivory Coast, alieleza imani yake ya kupata ushindi ni kubwa kwa sababu ya mambo makubwa mawili, nje na kikosi bora ambacho Simba wanacho kwa sasa.


“Mimi sio mgeni kabisa na ASEC nawajua na wananijua, kingine mazoezi tuliyofanya kabla ya safari hivyo vinanihakikishia kuanza kufunga mabao ugenini.


“Kitu kingine kinachonipa matumaini ya kushinda ni mechi nyingi za ligi tulizocheza kuliko wapinzani wetu hali iliyofanya miili yetu kuwa tayari zaidi kwa mashindano.


Muivory Coast huyo ni miongoni mwa maingizo mapya dirisha dogo msimu huu akitokea Green Eagles ya Zambia, alitua akiwa na rekodi ya kufunga mabao 12 katika mechi 17 alizocheza. Mechi tano za ligi amecheza jumla ya dakika 199, amefunga bao moja.


Ikumbukwe Simba katika mechi tano za mwisho haijapoteza mchezo hata mmoja ukiachana na sare moja dhidi ya Azam FC, huku ikishika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi 36, katika mechi 15 ilizocheza.


ASEC ambao sasa iko kileleni mwa kundi na pointi 10 ikifuatiwa na Simba yenye alama tano, nayo imecheza mechi 15 za ligi ikishika nafasi ya nne ikiwa na pointi 26, katika michezo minne ya mwisho imepoteza miwili na kushinda miwili akiwa katika uwanja wa nyumbani.