Arusha mjini wajiongeza

Muktasari:

  • ADFA wamefikia hatua hiyo baada ya TFF kupitisha kanuni za kutaka wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 ndio wacheze ligi ya wilaya Arusha mjini.

Baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitisha azimio linaloelekeza ligi za wilaya kuchezwa na vijana chini ya umri wa miaka 20, chama cha soka wilaya ya Arusha mjini (ADFA) wameamua kujiongeza kwa kubuni mashindano mapya yatakayohusisha timu za wanaume wenye umri mkubwa.

TFF wamepitisha azimio hilo kwenye mkutano wa 17 wa shirikisho hilo jijini mwanza mwaka huu kwa kile walichodai kusaidia , kuibua , kuvitengeneza, kuvikuza na kuviendeleza vipaji vya vijana  wengi nchini watakaoweza kuongeza wigo wa wachezaji kwa matumizi ya timu za Taifa.

Kutokana na hilo, chama cha soka wilaya ya Arusha mjini (ADFA) wamebuni mashindano kwa ajili ya vijeba hao walionekana kutengwa huku wakiyapa jina la 'Mega fm Arusha super cup'.  yatakayotekeleza kauli mbiu ya mwaka huu 'Mpira lazima uchezwe'.

Akizungumzia mashindano hayo, makamu mwenyekiti wa ADFA, Isabella Mwampamba alisema lengo kuu la michuano hiyo ni kuendeleza, kukuza na kuviendeleza vipaji vipya vya soka.

"Malengo mengine ya mashindano haya ni kukuza ushawishi kwa wadau kusapoti maendeleo ya soka la Arusha mjini lakini pia kujenga na kuimarisha afya za wachezaji na kujiepusha na makundi ya kihalifu" Alisema..

Alisema kuwa mashindano hayo waliyofanikiwa kupata udhamini wa kituo cha redio cha Mega fm, wameyaingiza kwenye kalenda yao, huku akiwaomba wadau wengine wajitokeze kusapoti maendeleo ya soka la Arusha mjini ikiwemo michuano mbali mbali ya watoto, veterani na ligi za wanawake.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya mashindano, Frank Luhohela alisema kuwa mashindano hayo yanatarajia kuanza kutimua vumbi mwanzoni mwa mwezi may mwaka huu yakihusisha timu zaidi ya 20 zilizoko ndani ya jiji la Arusha.

"Timu zote za jiji la Arusha tumezipa barua ya kuwaalika kushiriki mashindano haya zikiwemo za taasisi mbali mbali za elimu na soka, vijiwe vyote vya bodaboda Bajaji na daladala lakini pia timu binafsi hivyo tunatarajia timu zitaongezeka achilia mbali 20 zilizoonyesha nia"

Nae mwakilishi wa vilabu ADFA, Mwansasu Kabalika alisema kuwa zawadi kwa mshindi wa kwanza atajinyakulia kikombe kikubwa, na fedha taslim shilingi milioni moja, huku mshindi wa pili alizawadiwa 500,000.

"Zawadi zingine za fedha taslim zitaenda kwa mfungaji bora, kipa bora na kocha huku timu zitakazingia hatua ya robo fainali zikizawadiwa seti nzima ya jezi " alisema.

Kwa upande wake Meneja wa kituo cha redio Mega fm, Amani James alisema kuwa wameamua kudhamini mashindano hayo ili kusaidia kukuza soka la vijana wa Arusha ikiwa ni sehemu ya kurudisha shukrani kwa jamii kwa kukuza na  kuendeleza na vipaji lakini pia kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu kuifanya mpira kuwa kiwanda cha kuzalisha ajira nchini