Anayefuata Yanga anakula tano, ili Simba watie akili
Muktasari:
Tathmini hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha ambaye alisema safu yao ya ushambuliaji inayoundwa na viungo Simon Msuva, Deus Kaseke ambaye hubadilishana na kinda Geofrey Mwashiuya na washambuliaji Donald Ngoma na Amissi Tambwe ina kasi nzuri ya kufunga jambo ambalo ni muhimu katika kusaka ushindi wa timu.
UONGOZI wa Yanga umeridhishwa na kiwango cha timu yao lakini bosi mmoja ambaye kitaaluma ni kocha wa soka katoa kauli moja itakayowatisha wapinzani wowote watakaokutana na kikosi chao katika mechi zijazo wakisema bado kidogo tu kuna timu itapigwa bao tano mpaka sita.
Yanga imeng’ang’ania kileleni mwa msimamo wa ligi kama ilivyomaliza msimu uliopita wakiwa sawa kwa asilimia 100 wakishinda mechi zote mbili bila kuruhusu bao lolote sambamba na watani wao Simba lakini wakitofautiana kwa mabao ya kufunga.
Tathmini hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha ambaye alisema safu yao ya ushambuliaji inayoundwa na viungo Simon Msuva, Deus Kaseke ambaye hubadilishana na kinda Geofrey Mwashiuya na washambuliaji Donald Ngoma na Amissi Tambwe ina kasi nzuri ya kufunga jambo ambalo ni muhimu katika kusaka ushindi wa timu.
Bosi huyo akaongeza kwamba safu yao ya kiungo wa kati chini ya Haruna Niyonzima na Thabani Kamusoko ‘rasta’ inafanya kazi vyema ya kuzuia na kuchezesha timu na endapo itaongezewa nguvu kwa kurudi kwa mkabaji Said Makapu itakuwa bora zaidi ya sasa.
“Makocha wanafanya kazi nzuri kama uongozi tunaridhishwa lakini zaidi ni timu hasa wachezaji wanavyojituma na tunavyoiangalia timu yetu tunaona bado kuna nafasi kubwa ya kupata ushindi mkubwa zaidi,”alisema.
“Unawezaje kushangaa ukisikia Yanga imempiga mtu tano au sita mechi zijazo? Uwezo huo tunao lakini hata safu yetu ya ulinzi nayo inaonekana kuwa imara nimeshuhudia mechi mbili tulizocheza kipa wetu (Ally Mustapha Barthez) akiokoa mashambulizi mawili tu ya hatari, huo ni ubora wa mabeki wetu.”
Nahodha wa Prisons ambaye ni beki mkongwe Laurian Mpalile amevunja ukimya akisema walijipanga vyema kuwazuia Yanga baada ya kuwaona Mbeya walipocheza nao mechi ya kirafiki lakini safu ya ushambuliaji ya Yanga iliwashinda.
PLUIJM AFAFANUA
Mholanzi Hans Pluijm alisema: “Hii ndiyo Yanga ninayoihitaji, kwanza ni bandika bandua ukimtoa huyu, ukimwingiza mwingine anacheza mpira mzuri na anakushawishi hata mechi ijayo umwanzishe. Mfano ninavyowatumia, Ngoma na Tambwe kuanza, yule Busungu anapotokea benchi si kwamba hajui ninakuwa na malengo yangu na utaona mechi nyingine ataanza.”
“Lakini nashukuru kwa ushindani huo wa namba, kila nafasi ina wachezaji zaidi ya wawili na siyo mizigo wanajua na wenyewe kwa wenyewe wanapambana hali inayorahisisha kazi.”
Ushindani huo kuanzia ushambuliji ni Tambwe, Ngoma, Msuva na Geofrey Mwashiuya, Kaseke, Busungu, Mathew Simon na Mbrazili Andrey Coutinho.
Kiungo ni Niyonzima, Salum Telela, Kamusoko, Said Juma ‘Makapu’, beki ya kati yupo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Yondani, Mtogo Vincent Bossou, Pato Ngonyani, beki ya kulia, Mbuyu Twite, Juma Abdul, kushoto Haji Mwinyi, Oscar Joshua na makipa wapo Barthez, Deogratius Munishi ‘Dida’, Benedict Tonocco na Mudathir Hamis.
Pluijm ambaye anachezesha mabeki wanne nyuma, viungo watatu na washambuliaji watatu alisema: “Ninafurahi, lakini sitaki waridhike.”